Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri ameonyesha kuridhishwa kwake na makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni na Nishati wa nchi tatu za Misri, Sudan na Ethiopia kuhusiana na Bwawa la an-Nahdha.
Sameh Shoukry, alisema hayo jana mwishoni mwa kikao cha pamoja cha Misri, Ethiopia na Sudan kilichofanyika katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum. Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa pamoja na mawaziri wenzake wa Sudan na Ethiopia amesisitizia haja ya kuheshimiwa misingi iliyotangazwa mwezi Machi uliopita baina ya nchi tatu hizo. Ameongeza kuwa, pande husika zimesisitiza kwa uhakika kamili juu ya kufikiwa malengo ya kiistratejia, kuaminiana na kufikiwa makubaliano madhubuti zaidi katika kila hatua.
Mawaziri hao wametiliana saini " Hati ya Khartoum" ambayo ni matokeo ya mkutano wa siku tatu. Aidha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri, Ethiopia na Sudan wamekubaliana kushiriki katika duru nyingine mpya ya mazungumzo tarehe Mosi Februari ikiwashirikisha pia mawaziri wa nishati wa nchi hizo tatu kwa ajili ya kukamilisha hali ya kuaminiana baina ya nchi hizo. Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, kwa viongozi wa nchi hizo tatu kujitokeza na kuelezea kuridhishwa kwao na matokeo ya kikao chao. Vikao vilivyotangulia baina ya nchi hizo vilivunjika kutokana na pande husika kutofikia makubaliano.
Bwawa la an-Nahdha linajengwa na Ethiopia katika Mto Nile na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2017 na kuwa bwawa kubwa zaidi la uzalishaji umeme barani Afrika. Aidha kukamilika bwawa hilo kutalifanya liingie katika orodha ya mabwawa kumi makubwa zaidi ulimwenguni yanayozalishaji nishati ya umeme. Hii ni katika hali ambayo, Misri na Sudan zina wasiwasi mkubwa na ujenzi huo kutokana na hisa ya maji itakayotumika katika uzalishaji wa nishati ya umeme.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanauona mradi wa ujenzi wa Bwawa la an-Nahdha kuwa ni tishio kwa maslahi ya Misri kwa upande wa kisiasa na hata katika uga wa kiusalama. Wasiwasi wa serikali ya Misri ni mkubwa zaidi ukilinganishwa na wa Sudan. Hii ni kutokana na kuwa, sehemu ya sekta ya kilimo na takribani akiba yote ya maji ya nchi hiyo inategemea maji ya Mto Nile. Baadhi ya wachambuzi wa Misri wanaamini kuwa, ujenzi wa bwawa hilo ni njama ya Ethiopia yenye lengo la kuzusha mizozo na mivutano ya maji nchini Misri. Wachambuzi hao wanaamini kuwa, viongozi wa Ethiopia wanatumia vibaya mazingira mabaya yanayotawala hivi sasa nchini Misri na hali tete ya kisiasa ya miaka ya hivi karibuni ya nchi hiyo. Baadhi weledi wa mambo wanaashiria suala la vita vya kuwania maji hususan katika nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kuzungumzia nafasi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuisaidia Ethiopia kujenga Bwawa la an-Nahdha.
Wachambuzi wa mambo nchini Misri wanasema kuwa, endapo bwawa hilo litajengwa na kukamilika, wakulima milioni 10 wa nchi hiyo watakuwa wakimbizi na wakati huo huo Ziwa Nasser lililoko kusini mwa Misri litakauka. Hata hivyo Ethiopia inasisitiza kuwa, ina haki ya kutumia rasilimali zake kujiletea maendeleo. Maafikiano ya jana ya Khartoum yana umuhimu mkubwa kutokana na kuwa, baadhi ya wachambuzi wa mambo walikuwa wanatabiri kuwepo uwezekano wa kuongezeka mivutano baina ya nchi hizo endapo hakutafikiwa makubaliano kuhusiana na mzozo wa Bwawa la an-Nahdha.
0 maoni:
Chapisha Maoni