Umoja wa Afrika umeahidi kudumisha amani katika nchi wanachama wa umoja huo.
Hayo yamesemwa na Bi. Nkosazana Dlamini-Zuma, Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika katika ujumbe wake wa mwaka mpya wa 2016. Ameongeza kuwa, kwa ushirikiano na nchi za Burundi, Libya, Mali na Sudan Kusini, umoja huo umeahidi kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana katika nchi hizo.
Dlamini-Zuma ameongeza kuwa nchi hizo nne ni changamoto kubwa ya usalama kwa bara la Afrika.
Aidha amesisitiza kuwa, kamati maalumu ya uchunguzi ya Umoja wa Afrika kuhusu Sudan Kusini tayari imeshamaliza kazi zake na imetoa mapendekezo kuhusu amani, usalama, uadilifu na ustawi endelevu Sudan Kusini. Dlamini-Zuma amesema mwaka mpya wa 2016 utakuwa ni muhimu katika uga wa haki za binadamu barani Afrika na kuongeza kuwa, Umoja wa Afrika utajikita zaidi katika masuala ya kuimarisha elimu na kuinua kiwango cha haki za binadamu barani Afrika hasa haki za wanawake katika nchi za bara hilo. Amesema katika mwaka uliopita, bara la Afrika limepiga hatua na kupata mafanikio katika sekta za demokrasia na utawala bora na pia katika kupambana na ugonjwa hatari wa Ebola.
0 maoni:
Chapisha Maoni