Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametoa msamaha kwa wanachama sita wa harakati ya wanaotaka kujitenga na nchi hiyo huku akifuatilia sera za mazungumzo ya kitaifa kabla ya uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.
Televisheni ya taifa imetangaza kuwa wanachama tisa wa kundi linalopigana kujitenga la Bundi Dia Kongo (BDK) wamesamehewa na wataachiliwa huru kutoka jela walikokuwa wakitumikia vifungo vya maisha.
BDK ambayo inamaanisha Ufalme wa Kongo kwa lugha ya Kikongomani ni harakati inayopigania kujitenga baadhi ya maeneo ya kusini magharibi mwa nchi hiyo kubwa ya Afrika.
Kundi hilo linataka kurejeshwa ufalme wa jadi wa Kongo katika mipaka ya kabla ya ukoloni inayojumuisha baadhi ya maeneo ya Angola, Kongo na Gabon.
Wanachama hao wa Bundi Dia Kongo walihukumiwa kifungo cha maisha gerezani mwaka 2009 baada ya mapambano baina ya wafuasi wa kundi hilo na polisi ambapo watu 27 waliuawa.
Rais Kabila aidha ametoa msamaha kwa wafungwa walio na umri wa zaidi ya miaka 70. Waziri wa Sheria DRC Alexis Thambwe Mwamba amesema pia wafungwa wengine zaidi wataachiliwa kwa masharti kabla ya Januari 10. Kabila ambaye aliingia madarakani mwaka 2001 na kisha akashinda katika chaguzi za 2006 na 2011 ameitisha mazungumzo ya kitaifa kabla ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu. Katiba haimruhusu kugombea kipindi kingine lakini wapinzani wanamshutumu kuwa anapanga kutangaza kuwania tena kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu. Hata hivyo wafuasi wake wanasema Kabila analenga kutuliza hali ya mambo nchini humo kabla ya kuachia ngazi.
0 maoni:
Chapisha Maoni