Jeshi la Iraq limetangaza kuwa, vikosi vya nchi hiyo vimefanikiwa kuukomboa kikamilifu mji wa Ramadi, kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Jeshi hilo limewapongeza wananchi wote wa Iraq kufuatia kukombolewa makao makuu hayo ya mkoa wa al Anbar na kusema kuwa, vikosi vya Iraq vimefanikiwa kuingia katikati ya mji Ramadi baada ya kukomboa zaidi ya maeneo 30 ya mji huo.
Jeshi hilo limeongeza kuwa, bendera za Iraq zimepeperushwa kwenye majengo ya serikali baada ya kusafishwa maeneo yote ya mji huo yaliyokuwa yametegwa mabomu kila mahali.
Meja Jenerali Yahya Rasul, mmoja wa makamanda wa jeshi la Iraq amesema kupitia televisheni ya nchi hiyo kuwa, Ramadi imeshakombolewa na kwamba askari wa vikosi maalumu vya kupambana na ugaidi wamepeperusha bendera ya Iraq kwenye majengo ya serikali.
Ramadi ni mji muhimu sana ulioko umbali wa kilomita 110 kutoka mjini Baghdad. Makao makuu hayo ya mkoa wa al Anbar yalitekwa na magaidi wa Daesh mwezi Mei 2015.
0 maoni:
Chapisha Maoni