Uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati umesogezwa mbele kwa siku tatu kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiufundi na sasa utafanyika tarehe 30 mwezi huu. Catherine Samba-Panza, Rais wa serikali ya mpito ya nchi hiyo ametangaza kuwa, raundi ya kwanza ya uchaguzi wa Rais na Bunge iliyokuwa imepangwa kufanyika Jumapili ya jana tarehe 27 sasa itafanyika Jumatano ijayo ya tarehe 30 Desemba.
Rais Samba-Panza ametangaza kuakhirishwa uchaguzi huo baada ya mkutano wake na wajumbe wa asasi za serikali ya mpito na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa. Ugumu katika upelekaji wa masanduku ya kupigia kura katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na kutolewa ripoti za kuuzwa makaratasi ya kupigia kura ya uchaguzi wa Rais na Bunge ni miongoni mwa sababu za kuakhirishwa uchaguzi huo. Uchaguzi huo ulitangazwa kuwa ungefanyika Jumapili ya jana katika hali ambayo, wachambuzi wa mambo walitangaza mara kadhaa kwamba, hakuna mazingira mazuri ya kuweza kufanyika uchaguzi huo katika tarehe iliyopangwa. Ripoti zinasema kuwa, makaratasi ya kura yamezagaa na kwamba, kuna baadhi ya watu wana makaratasi mawili hata matatu ya kupigia kura ambayo wameyapata kwa njia za magendo. Kabla ya hapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati alitangaza kujiuzulu kutokana na kile alichokieleza kuwa, kuweko mashinikizo mengi ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa hali yoyote ile kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2015.
Licha ya kushadidi vurugu na machafuko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, lakini juma lililopita wananchi wa nchi hiyo walishiriki katika kura ya maoni ya katiba. Viongozi wa nchi hiyo wanasema kuwa, ushiriki wa wananchi ulikuwa mzuri na kwamba, huo ni utangulizi wa kufanyika uchaguzi wa Rais na ule wa Bunge. Pamoja na hayo, suala la kuweko udanganyifu na kuandaliwa mazingira ya uchaguzi kwa manufaa ya mgombea fulani ni jambo ambalo kwa muda sasa limekuwa likizungumziwa na weledi wa siasa za nchi hiyo.
Wajuzi hao wa mambo wamekwenda mbali zaidi na kusema kuwa, hata wafanyakazi wa vituo vya kupigia kura akthari yao bado hawajapata mafunzo ya lazima kwa ajili ya kazi hiyo.
Umoja wa Afrika AU unatarajiwa kutuma ujumbe wake wa watu 30 kwa ajili ya kwenda kusimamia uchaguzi huo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Waangalizi hao wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika wana jukumu la kutathmini namna uchaguzi huo ulivyoandaliwa, utakavyofanyika, haki sawa katika upigaji kura na itibari ya uchaguzi huo na kisha kutoa ripoti yao katika mkutano na waandishi wa habari.
Rais wa mpito Bi Catherine Samba-Panza ambaye amekuwa madarakani tangu Januari mwaka jana ana matumaini kwamba, kufanyika uchaguzi huo kutahitimisha muda wa serikali ya mpito na kwa kuingia madarakani serikali mpya iliyochaguliwa na wananchi, vurugu na machafuko nayo yatakomeshwa na hivyo wananchi kushuhudia tena amani na utulivu.
0 maoni:
Chapisha Maoni