Makundi hasimu ya kisiasa ya Burundi leo Jumatatu yamenza duru mpya ya mazungumzo ya amani katika mji mkuu wa Uganda Kampala.
Wawakilishi wa serikali ya Bujumbura na muungano wa vyama vya upinzani na wawakilishi wa jumuiya za kiraia wanashiriki katika mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la mazungumzo hayo ni kutafuta suluhisho la amani la mgogoro wa Burundi.
Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa ndani mapema mwaka huu baada ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kutangaza nia ya kugombea tena kiti hicho kwa muhula mwingine wa tatu mfululizo. Wakati huo wapinzani wa Nkurunziza walipinga uamuzi huo wakisema unakiuka katiba na makubaliano ya amani ya Arusha yaliyokomesha vita vya ndani hapo mwaka 2006.
Serikali ya Bujumbura ilikuwa ikikataa kushiriki katika maungumzo hayo ya amani. Rais Nkurunziza anaamini kuwa, muungano wa vyama vya upinzani na jumuiya za kiraia ni makundi ya kigaidi ambayo yalihusika na jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali yake mwezi Mei mwaka huu na kwamba walihusika na mashambulizi kadhaa yaliyolenga vituo na kambi za jeshi mjini Bujumbura. Jumuiya za kutetea haki za binadamu zinasema watu 154 waliuawa katika mashambulizi hayo na wengine 150 hawajulikani waliko.
Machafuko na hali ya ukosefu wa usalama katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura imewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa nchi jirani ambao wametaka kufanyike mazungumzo ya amani ya Kampala. Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao wana wasiwasi wa kutokea vita kamili vya ndani na mauaji ya kimbari nchini Burundi wamekuwa wakisisitiza sana udharura wa kufanyika mazungumzo kati ya pande mbili hasimu. Muundo wa kijamii wa Burundi unaofanana sana na ule wa Rwanda umezidisha wasiwasi wa nchi jirani na jamii ya kimataifa kuhusu uwezekano wa kutokea mauaji ya kimbari nchini humo kama yale yaliyotokea mwaka mwaka 1994 nchini Rwanda.
Kutokana na hali hiyo Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limependekeza suala la kutumwa askari wa kulinda amani nchini Burundi kwa shabaha ya kushirikiana na nchi hiyo. Ijumaa ya Disemba 25 wanachama wa baraza hilo walipasisha azimio la kutuma askari 5000 na wameipa serikali ya Bujumbura muhula wa siku saba kupasisha suala hilo. Umoja wa Afrika unasisitiza kuwa, lengo la kutumwa askari hao nchini Burundi ni kulinda maisha ya raia kutokana na ukatili na ghasia zinazoendelea nchini humo. Hata hivyo muungano unaotawala unasema, kuwepo askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini humo kutakiuka mamlaka ya kujitawala. Kwa msingi huo wafuasi wa muungano huo wamefanya maandamano mjini Bujumbura wakilaani uamuzi wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi na viongozi waandamizi wa muungano unaotawala wanachochea hisi za utaifa kwa ajili ya kuzuia uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kutuma askari wa kulinda amani nchini humo.
Maafisa wa usalama wa serikali ya Burundi wanadai kuwa, machafuko ya sasa nchini humo yanatokea katika sehemu ndogo tu ya jiji la Bujumbura na kwamba hali ni shwari katika maeneo mengine yote ya nchi hiyo. Hata hivyo yanayojiri nchini humo na ripoti mbalimbali za mashirika ya kutetea haki za binadamu yanatoa ripoti tofauti kuhusu hali ya Burundi.
Ala kulli haal, duru za kisiasa na taasisi za kutetea haki za binadamu zinatarajia kuwa, duru mpya ya mazungumzo ya amani nchini Burundi inayofanyika chini ya usimamizi wa Rais Yoweri Museveni itakuwa hatua muhimu ya awali katika njia ya kukomesha kabisa machafuko na mgogoro wa sasa nchini humo.
0 maoni:
Chapisha Maoni