Jumatano, 23 Oktoba 2013

Yanga, Simba zagawa vigogo wa Serikali Dar

SARE ya mabao 3-3 baina ya Simba na Yanga katika mchezo wa juzi Jumapili, imefichua ushabiki wa vigogo wengi wa siasa na watu maarufu nchini waliokuwapo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kushuhudia mchezo huo.
Jukwaa Kuu sehemu ya watu maalumu, lilikuwa limesheheni vigogo wa Serikali, vyama vya siasa, waigizaji filamu, makamanda wa polisi, wafanyabiashara na wanamichezo kadhaa maarufu.

Wakati dakika 45 za kipindi kwanza zilipokatika huku Yanga ikiwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyotiwa kimiani na Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza (mawili), baadhi ya vigogo waliwazodoa wenzao wa Simba ambao ilibidi wanywee.

Waliokuwa wakitamba ni pamoja na Kapteni Geoge Mkuchika (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora), Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema), Yusuf Manji (Mwenyekiti wa Yanga), Ridhiwani Kikwete (Mtoto wa Rais wa Tanzania) na Steve Nyerere (Mwigizaji Filamu).

Ili kuwamaliza nguvu wenzao wa Simba, vigogo hao walionekana kukumbatiana kwa furaha huku Manji akipita huku na huko akipunga mikono kwa mashabiki wa Yanga jambo lililokoleza hamasa uwanjani hapo kwa muda. Lakini baada ya Simba kuanza kurejesha mabao hayo kipindi cha pili na kusawazisha kupitia kwa Betram Mwombeki, Gilbert Kaze na Joseph Owino, vigogo wa Yanga walinywea na wale wa Simba wakachukua nafasi ya kutamba.

Wanazi hao wa Simba waliongozwa na Ezekiel Maige (Mbunge wa Msalala), Charles Kenyela (zamani Kamanda wa Polisi Kinondoni) na wengineo kadhaa ambao walijibu mapigo kwa kuwadhihaki wale wa Yanga waliolazimika kuinamisha vichwa wakiwa hawaamini kile walichokuwa wanakiona.
Hadi mchezo unamalizika kwa sare hiyo, wale wa Yanga ni kama hawakuamini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top