Madogo wa Simba walioiua Yanga
YANGA
itajutia sare ya mabao 3-3 dhidi ya Simba, lakini ukweli halisi ni
kwamba, viungo vijana wa Wekundu hao wa Msimbazi, Said Ndemla na William
Lucian ‘Gallas’ ndiyo waliiamsha Simba ikasawazisha mabao yote matatu.
Gallas na Ndemla wote kwa pamoja waliingia dakika
ya 46 kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Abdulhalim Humoud na Haroun
Chanongo waliokuwa wameanza kipindi cha kwanza.
Wachezaji hao ambao wanachipukia kwenye Ligi Kuu
Bara na hawana uzoefu na mechi kubwa kama hiyo licha ya msimu uliopita
kutumiwa kwenye baadhi ya mechi na kocha Mfaransa Patrick Liewig.
Jumapili iliyopita, Simba walishikika kipindi cha
kwanza, wakafungwa mabao matatu ya haraka haraka lakini walipoingia
vijana hao hawakufanya makosa, waliibadilisha timu kabisa.
Makosa ya awali yaliyotokana na safu ya kiungo
iliyokuwa na Humoud ambaye alicheza kiungo mshambuliaji mbele ya Jonas
Mkude aliyekuwa kiungo mkabaji hayakujitokeza tena, badala yake Simba
ikashika usukani na mpira ukachezwa Msimbazi.
Ndemla
Ndemla ambaye anacheza kwa mara ya kwanza mechi
ngumu kama hiyo amesema: “Ni mara ya kwanza kucheza mechi ngumu kama
hii, lakini kwa sababu niliusoma mchezo kabla sijaingia, ikawa rahisi
kwangu. Nikaingia uwanjani na matumaini na sikuhofu kitu na zaidi baada
ya kuona benchi la ufundi linaniamini.”
Alikiri kuwa kabla ya kuingia yeye na Gallas aliona safu ya kiungo chao kilikuwa kimepwaya.
“Niliona Athuman Idd ‘Chuji’ na Frank Domayo ndiyo
kizuizi kwetu, wao ndiyo walipandisha sana mashambulizi na kuwapa
nafasi washambuliaji wao watushambulie kwa urahisi na nilipoingia
nilipambana nao, namshukuru Mungu mambo yalienda vizuri,”anafafanua
Ndemla aliyeweka wazi anajisikia mwenye furaha kubwa.
Ndemla mwenye miaka 19, sifa yake kubwa anajua
kubadilisha mchezo anapotokea benchi, ana akili ya mpira na sugu anaweza
kuingia mahali popote kwenye ugumu.
Simba imempandisha, Ndemla kutoka kikosi chao cha
timu ya vijana na kumpa majukumu hayo lakini anapata ugumu kuonekana
zaidi kutokana na ushindani wa namba uliopo kwa sababu Simba ina viungo
wengi kama, Gallas, Abdallah Seseme, Mkude, Ramadhani Chombo ‘Redondo’,
Humoud na Kiemba ingawa ametamka kuwa ana uwezo wa kucheza namba
nyingine na kumudu vizuri kama winga ya kulia na namba 10.
“Simba ni timu kubwa yenye ushindani wa juu hasa
nafasi ya kiungo ina wachezaji wengi, hiyo ndiyo changamoto kwangu
inayonifanya nijitume kwa nguvu zote kuhakikisha napata nafasi kikosi
cha kwanza,”anaeleza Ndemla anayeipenda klabu ya Chelsea ya England.
0 maoni:
Chapisha Maoni