Kaburu ajinadi ujumbe wa TFF
WAKATI uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF)
umepangwa kufanyika Jumapili, Mjumbe wa Bodi ya Ligi, Geofrey Nyange
‘Kaburu’, amesema atahakikisha Ligi Kuu Bara inapata udhamini mnono
zaidi msimu ujao.
Kaburu anayewania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupitia Kanda Namba 12 (Pwani na Morogoro), alisema ataendeleza harakati zake za kupigania masilahi ya ligi hiyo ili kupata wadhamini wengi zaidi na kuyafanya mashindano hayo kuwa bora zaidi.
Kaburu ndiye aliyeanzisha harakati za kuipigania ligi hiyo kuwa huru, harakati ambazo zilizaa matunda kwa kuanzishwa Bodi ya Ligi Kuu ambayo viongozi wake wa kwanza watapatikana Oktoba 25.
Kaburu alisema soka si lelemama, inahitajika fedha na uwekezaji wa hali ya juu ikiwamo kuishirikisha Serikali ipasavyo.
“Lazima kuwe na mpango mkakati, si kila anayeingia awe na mkakati wake, lazima tuwe na mipango ya muda mrefu na mfupi, tuwe na malengo kuanzia mwaka huu mpaka mwaka fulani tuwe tumeshafanya moja, mbili, tatu. Hata kama mtu anaondoka, anayeingia basi aendeleze pale alipoishia wa kwanza,” alisema.
“Wadau ni lazima washirikishwe ili kufikia
malengo, mdau mkuu ni Serikali, ndiyo inayopaswa kuweka dira ya
kuwaendeleza vijana kuanzia shuleni, ikiwa ni pamoja na vituo vya
kuendeleza vipaji.”
0 maoni:
Chapisha Maoni