Maalim Seif akiongea kuhusu sakata la Lipumba |
Sarakasi za kisiasa zinaendelea kutawala ndani ya chama cha CUF baada ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kudai kuwa Profesa Ibrahim Lipumba anatumiwa kukihujumu chama hicho.
Maalim Seif alimtuhumu Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa
CUF, anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa
anakihujumu chama ili kishindwe kudai haki waliyoipata katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25 mwaka juzi.
Aliyasema hayo katika kijiji cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini
Unguja alipozungumza na wanachama wa chama hicho, ikiwa ni ziara maalumu ya
uimarishaji wa chama katika mikoa yote ya Kisiwa cha Unguja.
Maalim Seif alisema pamoja na Profesa Lipumba kupata nguvu
kutoka vyombo vya dola na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kukihujumu
chama hicho, lakini hawataweza kufikia malengo hayo.
Alisema taasisi hizo kwa pamoja zimekuwa zikimuunga mkono
Lipumba kwa kumpa kila nguvu anayohitaji ili kuona anafanikisha malengo ya CCM
ya kuitawala nchi bila ya kuwepo kwa chama kikuu pinzani, ila nguvu zao hizo
zitagonga mwamba.
Alishangazwa kuona Ofisi ya Msajili kwa kushirikiana na vyombo
vya dola badala ya kufuata Katiba na sheria za nchi, wao wamekuwa wakikihujumu
chama hicho.
Kuhusu kuondolewa kwenye nafasi yake, Maalim Seif alisema kwa
mujibu wa katiba ya CUF, Lipumba hana uwezo wa kumvua nyadhifa hiyo hata kama
angekuwa ni mwenyekiti halali.
Alisema kwa mujibu wa katiba yao ili Katibu avuliwe wadhifa wake
lazima mkutano mkuu uhudhuriwe na zaidi ya nusu ya idadi wajumbe.
Alisema kikao kilichofanyika chini ya Profesa Lipumba
kilihudhuriwa na wajumbe wasiokuwa na ujumbe kihalali, ambao walipandikizwa
kuonesha kama kikao hicho kilikuwa halali.
Maalim Seif alisema kuwa kinachosikitisha ni kuona Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa nayo kuidhinisha kuwa wamekubaliana na mageuzi hayo
yaliyofanywa na Lipumba kwa kushirikiana na wajumbe wake.
Akizungumzia madai ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliopita, Maalim
Seif alisema waliwataka wananchi wa Zanzibar kutokata tamaa na haki yao, huku
akidai hivi karibuni dola ya Zanzibar itakuwa chini ya CUF.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema
uongozi wa CUF unasikitika kuona vyombo vya dola vikiingilia mamlaka ya chama hicho na kusahau wajibu wao.
Alisema kuwa wajibu wa vyombo hivyo ni kusimamia amani ya
wanachama na viongozi wake, lakini ni jambo la kushangaza kwa viongozi wa
vyombo hivyo kuwa ni miongoni mwa wanaongoza kuonesha chuki dhidi ya CUF.
Alisema pamoja na hujuma hizo, lakini viongozi wakuu wa chama
hicho chini ya Maalim Seif, hawatosita kudai haki yao hadi kieleweke.
Akijibu tuhuma hizo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara na
anayemuunga mkono Profesa Lipumba, Magdalena Sakaya alimtuhumu Maalim Seif kuwa
ndiye anakula njama za kukidhoofisha chama.
Alisema Seif amekataza ruzuku zisifike kwenye wilaya, hakuna
mikutano na hakuna hata pikipiki huku wenzao Chadema waliokuja juzi wamekuwa
chama kikuu cha upinzani kutokana na kuwa wamoja.
Alieleza kuwa badala ya kujenga chama, ameamua kukidhoofisha na
anatumiwa kufanya hivyo akijificha kwenye mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
0 maoni:
Chapisha Maoni