Ikiwa ni takribani miaka mitano tangu Mbunge wa Kigoma Mjini,
Zitto Kabwe, avurugane na Chadema ambacho kilikuwa chama chake, sasa hali hiyo
inaonekana kurudi tena kupitia uchaguzi wa ubunge wa Afrika Mashariki (EALA).
Tofauti na awali ambapo alikosana na Chadema na kufukuzwa
uanachama kutokana na kile kilichodaiwa ni kuandaa waraka wa mabadiliko ya
2013, sasa hivi ubunge wa EALA unaonekana kumvuruga tena mwanasiasa huyo na
Chadema, baada ya kuandika barua kwa Spika wa Bunge akitaka utaratibu
uliotangazwa wa namna ya kupata wabunge ubadilishwe.
Utaratibu huo mpya uliotangazwa, unatoa nafasi kwa wabunge wa
EALA kwa mwaka 2017 kulingana na idadi ya wabunge wa kila chama kwenye Bunge la
Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa Mwongozo huo, kutokana na idadi ya wabunge wa
vyama kwa kila chama, CCM imepata nafasi za wabunge sita kwenda EALA, Chadema
mbili, CUF moja, huku ACT Wazalendo pamoja na NCCR Mageuzi, vikiwa havina
nafasi hata moja kwenye Bunge hilo la Afrika Mashariki, kutokana na kuwa na
mbunge mmoja kila kimoja, hivyo kutokidhi vigezo.
Kutokana na hali hiyo, Zitto ameliandikia Bunge barua kutaka
Kamati ya Kanuni za Bunge ikutane kujadili uchaguzi wa wajumbe wa Tanzania
kwenye Bunge la Afrika Mashariki.
Barua hiyo, ambayo baadhi ya wachambuzi wa siasa wanadai
inalenga kutaka utaratibu wa awali ubadilishwe ili chama cha Zitto (ACT
Wazalendo), kimwingize mwanachama wake, Profesa Kitila Mkumbo kugombea ubunge
huo, inasema mwongozo uliotolewa na Bunge umekwenda kinyume cha Mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wanasema endapo hoja ya Zitto ikikubaliwa, ni rahisi zaidi
wagombea wa Chadema wakakosa nafasi hizo na badala yake nafasi za upinzani
kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki zikachukuliwa na
wagombea wa ACT na wale wa CUF.
Hali hiyo inaelezwa kuchangiwa na wabunge wengi kwenye Bunge la
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kuwa ni wa CCM, hivyo ni rahisi kuweka msimamo
wa kuwapigia kura wale wagombea wa ACT Wazalendo na wale wa CUF, badala ya wale
wa Chadema kutokana na hali ya kisiasa iliyopo nchini kwa sasa.
Barua ya Zitto ya Machi 28 iliyoandikwa kutokana na Tangazo la
Bunge kwenye gazeti namba 11 la Machi 17, lililotangaza uchaguzi huo na
masharti yake, ilisema mwongozo wa uchaguzi huo unavunja kanuni mbalimbali na
kwamba kitakachofanyika sasa kitakuwa ni uteuzi na siyo uchaguzi.
Alisema pia mwongozo huo, mbali na kuvunja Mkataba wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, unataka suala la jinsi lizingatiwe kwenye wabunge wanaokwenda
kuiwakilisha nchi katika Bunge hilo.
Baada ya Zitto kuandika malalamiko hayo, Mwanasheria wa Chadema,
John Malya, naye aliyajibu akirejea hukumu mbili za kesi ya Anthon Komu (kwenye
Divisheni ya Mwanzo na Divisheni ya Rufani).
Malya aliandika kwamba, mwongozo wa Ofisi ya Spika wa Bunge wa
kugawa idadi ya viti kwa vyama ni sahihi, kwa sababu Divisheni zote mbili za
Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ziliamua.
Katika sehemu ya barua yake, alisema: “Mwenye kupaswa kubeba
mzigo wa makundi ya Zanzibar, Bara na Wanawake (ukiachilia mbali kundi la vyama
vya upinzani) ni chama chenye wabunge wengi (CCM)”.
Hoja hiyo ya Malya inachambuliwa na Ado Shaibu, ambaye aliandika
ujumbe unaogusa hoja za kisheria ambazo alitumia Malya kukosoa malalamiko ya
Zitto.
Shaibu alisema ni kosa kutumia kesi ya Antony Komu ambayo
iliamuliwa na Divisheni ya Mwanzo ya Mahakama ya Afrika Mashariki, lakini
baadaye Divisheni ya Rufani ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ikatengua
hukumu hiyo kwa hoja ya kwamba Divisheni ya Mwanzo ya Mahakama haikuwa na
mamlaka ya kuamua suala husika.
0 maoni:
Chapisha Maoni