Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kupiga kambi katika Kata ya Miono wilayani Bagamoyo na kuwasaka wafugaji wanaopiga wakulima.
Waziri mkuu alitoa agizo hilo alipozungumza na wakazi wa kata hiyo hivi karibuni alipokwenda kukagua miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
waziri mkuu waTanzania |
Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema diwani wa Miono, Juma Mpwimbwi akiwasilisha kero zao kwa kiongozi huyo alisema wanakabiliwa na tatizo la wakulima kupigwa na wafugaji na wakipelekwa kituo cha polisi hawachukuliwi hatua.
“Wafugaji wanatupiga lakini wenzetu hawachukuliwi hatua na hata ukienda kushtaki polisi hawakai kwa sababu wanadai wao wana fedha,”alisema diwani huyo.
Pia, alisema waliahidiwa barabara ya lami tangu miaka saba iliyopita, lakini hadi sasa hawana hata kipande kidogo tu cha barabara hiyo.
Mkazi wa kata hiyo, Shabani Mkwimbi akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake alisema wana kituo cha polisi na mahakama, lakini utendaji kazi wa viongozi waliopo unatia shaka.
Alimlalamikia mkuu wa kituo cha polisi na hakimu akidai wafugaji pekee ndiyo wanaoshinda kesi.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwahakikishia wakazi hao kwamba hakuna hata mtu mmoja ambaye yuko juu ya sheria. Alisema suala la polisi litashughulikiwa na kamanda wa mkoa.
Majaliwa alisema msimamo wa Serikali ni kuwaona wakulima na wafugaji wanafanya kazi zao kwa uhuru.
“Hakuna mfugaji anayeruhusiwa kupeleka ng’ombe kwenye mashamba yenye chakula. Mkuu wa mkoa hili ni agizo, njoo upige kambi hapa na watu wako, na usake wahusika hadi wabainike. Ni lazima tuwajue ni kina nani wamehusika na hili,” alisema.
0 maoni:
Chapisha Maoni