Burundi yatangaza kuutambua rasmi muungano wa upinzani wa ADC - Ikibiri
Edouard Nduwimana Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi amesema kuwa,
serikali ya Bujumbura imeutambua rasmi muungano wa vyama vya upinzani
nchini humo. Nduwimana amesisitiza kuwa, muungano wa Alliance of
Democrats for Change – Ikibiri 'ADC' ambao unaundwa na vyama vinne vya
upinzani unatambuliwa rasmi nchini humo. Licha ya serikali kuutambua
rasmi muungano huo, Leonce Ngendakumana kiongozi wa muungano huo
ameikosoa vikali serikali ya Burundi na kusema kwamba, uamuzi huo wa
serikali umetolewa kwa kuchelewa mno. Muungano wa ADC uliundwa na kutuma
nyaraka zake serikalini yapata miaka minne iliyopita. Wataalamu wa
masuala ya kisiasa wameeleza kuwa, huenda serikali ina malengo maalumu
kwa kutangaza kuutambua rasmi muungano wa ADC- Ikibiri, wakati huu ikiwa
imesalia miezi michache kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini
humo. Wadadisi wa mambo wanaeleza kuwa, uamuzi huo wa serikali ya
Bujumbura umechukuliwa kwa lengo la kupunguza migogoro na mikwaruzano
wakati huu wa kuelekea kwenye zoezi la uchaguzi wa rais. Uchaguzi mkuu
nchini Burundi umepangwa kufanyika mwezi Juni 2015, na utasimamiwa na
wasimamizi wa kimataifa. Rais Pierre Nkurunziza ambaye anabanwa kisheria
wakati akikaribia kumaliza muhula wake wa pili wa uongozi wa miaka
miaka mitano – mitano, bado hajatangaza rasmi kama ataondoka madarakani
au la. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Burundi imekuwa
ikikabiliwa na tuhuma kadhaa za taasisi za kimataifa za kuwabana na
kuwakandamiza wapinzani. Jeffrey Feltman Msaidizi wa Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa alisitiza juu ya kuwepo anga na mazingira huru ya
kisiasa kwa lengo la kudumisha amani na utulivu nchini humo. Inaonekana
kuwa, hatua ya kupigwa marufuku maandamano nchini humo, imewatia
wasiwasi viongozi wa jumuiya na taasisi za kimataifa. Kabla ya hapo,
jeshi la Burundi lilitangaza kupambana vikali na kundi lolote
litakalothubutu kuwashawishi wananchi waingie barabarani na kufanya
maadamano. Feltman amevitaka vyama vya upinzani kuelezea kinagaubaga
mitazamo yao kwa lengo la kutatua kwa amani mivutano na migogoro ya
kisiasa iliyoko nchini humo. Wadadisi wa mambo wanaeleza kuwa, kuwepo
hitilafu na migongano ya kisiasa kati ya viongozi, kushindwa kufanyika
mazungumzo ya kitaifa, ghasia na machafuko yanayosababishwa na umilikaji
wa ardhi na kuwaingiza vijana jeshini, ni miongoni mwa changamoto kuu
zinazotishia kuitumbukia nchini hiyo kwenye machafuko. Wadadisi hao
wameeleza kuwa, kasoro zilizojitokeza kwenye zoezi la uandikishaji wa
daftari la kudumu la kupigia kura ni miongoni mwa masuala
yanayolalamikiwa na wapinzani nchini Burundi. Vyama vya upinzani
vinaituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kukipendelea chama tawala cha
CNDD – FDD. Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa, hatua ya
serikali ya Burundi ya kuutambua rasmi muungano wa ADC italeta taathira
chanya katika kuboresha hali ya kisiasa nchini humo. Bila shaka,
kushadidi hitilafu na mivutano katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi
mkuu, kunaweza kusababisha kukaririwa vita na mapigano mapya ya wenyewe
kwa wenyewe nchini humo.
0 maoni:
Chapisha Maoni