Niger yatangaza maombolezo ya kitaifa ya siku tatu
Serikali ya Niger imetangaza maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku tatu na bendera zote nchini humo kupepea nusu mlingoti, baada ya kuuawa wanajeshi 9 wa nchi hiyo waliokuwa kwenye operesheni ya kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani kaskazini mwa Mali.Uamuzi huo umetangazwa baada ya kumalizika kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika chini ya uenyekiti wa Rais Mahamadou Issoufou wa Niger. Serikali ya Niger imesisitiza kwamba wanajeshi wa nchi hiyo walioko Mali wataendelea kupambana na makundi ya kigaidi hadi utakapokomeshwa uhalifu nchini humo. Rais Mahamadou Issoufou amesema kuwa, shambulio lililofanyika siku ya Ijumaa dhidi ya wanajeshi wa Niger haliwezi kudhoofisha mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, tokea mwezi Agosti mwaka huu Niger ilipeleka kundi la wanajeshi 850 nchini Mali kwa lengo la kurejesha amani na utulivu, chini ya mwavuli wa vikosi vya kimataifa vya kulinda amani.
0 maoni:
Chapisha Maoni