Jumanne, 19 Agosti 2014

Marekani yaendelea na mashambulizi Iraq

 Rais Barack Obama ameahidi kuisaidia serikali ya Iraq kupambana na waasi wa Dola ya Kiislamu ama IS. Wakati huo huo maelfu ya watu wanayakimbia makaazi yao kwa kuogopa kuuliwa na wapiganaji hao.


Ndege za kijeshi za Marekani zimeshambulia ngome kadhaa za wapiganaji wa kundi linalojiita Dola ya Kiislamu kaskazini mwa Iraq, linalotawaliwa na serikali yenye utawala wa ndani ya Kurdistan. Wapiganaji wa Kimarekani wanaripoti kwamba wamefanikiwa kulikomboa bwawa la Mosul ambalo ni kubwa zaidi nchini Iraq. Pamoja na hayo mashambulizi yalilenga pia magari na nyumba za wapiganaji wa IS.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Washington, Rais Barack Obama aliahidi kushirikiana na serikali ya Iraq. "Mapambano haya yatachukua muda. Tutakutana na changamoto nyingi," alisema Obama. "Lakini hakuna shaka kwamba Marekani itaendelea na operesheni za kijeshi nilizoziidhinisha."
Maelfu wakimbilia milimani
Obama ameahidi pia kushirikiana na nchi washirika kama vile Uingereza, Canada na Ufaransa kufikisha misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa haraka. Umoja wa Mataifa unakisia kuwa Wairaq zaidi ya laki sita wameyakimbia makaazi yao kwa kuogopa mapigano. Wengi wao wamekimbilia kwa ndugu wanaoishi katika maeneo yaliyo salama. Wengine wametafuta hifadhi katika kambi za Umoja wa Mataifa. Mmoja wao ni kijana Zidan. Ana miaka 12 na alikimbia nyumbani baada ya wapiganaji wa IS kuuvamia mji aliokuwa akiishi. "Tuliacha kila kitu na kukimbilia mlimani. Tumeacha nyumba yetu. Tulilala chini ya miti. Hatukuwa na nguo za kuvaa, " anaeleza Zidan. "Hatukuwa na kitu chochote mpaka tulipofika hapa. Tulikutana na watu wengi waliogaragara barabarani kwa sababu walikuwa na kiu. Walituomba maji ya kunywa lakini hatukuwa na maji."
Hivi sasa yapo makundi makuu matatu yanayopambana na waasi wa IS: Wanajeshi wa Marekani, wanajeshi wa Iraq na wapiganaji wa Kikurdi. Mwaka uliopita IS ilijitenga na kundi la kigaidi la al-Qaida. Nia ya IS ni kuanzisha utawala wenye kufuata msimamo mkali wa Kiislamu nchini Iraq na Syria. Kinachofanya IS kuwa tishio kubwa ni kwamba kundi hilo limekuwa likiuwa raia kikatili bila sababu yoyote. Ukatili huo umewafanya hata wanajeshi wa Iraq waweke silaha chini katika baadhi ya miji na kukimbia. Baadhi ya mataifa ya Magharibi yanajadili uwezekano wa kutuma silaha kwa wapiganaji wa Kikurdi ili waweze kukabiliana na IS.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa/afp
Mhariri: Mohammed Khelef
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top