BRAZIL 2014: Kwanini Brazil ilifungwa mabao saba?
HAKUNA uchawi katika soka la kisasa. Uwe ulilitazama pambano la
Brazil na Ujerumani ukiwa Tanzania au hapa Brazil, ilikuwa rahisi
kugundua kwa nini Brazil imefungwa mabao 7-1 na Ujerumani.
Hakukuwa na maajabu yoyote zaidi ya mbinu mbovu za
Kocha, Luis Fillipe Scolari. Katika soka la kisasa unaweza kufungwa
mabao mengi ndani ya dakika chache tu kama kocha anatumia mbinu mbovu
dhidi ya timu makini kama Ujerumani.
Wakati pambano linaanza, Scolari alikuwa ana
wachezaji wawili tu eneo la kiungo ambao ndio aliwaamini kuleta uwiano
katika ulinzi na mashambulizi.
Alikuwa na Luiz Gustavo na Fernandinho.
Wengine pale mbele walikuwepo Oscar, Bernard, Hulk
na Fred. Lilikuwa jambo la hatari sana kwa sababu wote hawa wana mawazo
ya kushambulia zaidi kuliko kujihami.
Mbaya zaidi kwa Scolari, alikuwa anacheza na timu
yenye viungo maridadi ambao klabu zao mbili; Bayern Munich na Borussia
Dortmund, zimetesa mno barani Ulaya katika miaka ya karibuni.
Unacheza dhidi ya Ujerumani iliyojaza viungo wengi
katikati akina Thomas Muller, Bastian Shweinsteiger na Toni Kroos. Hapo
hapo kuna Mesut Ozil wa Arsenal na Sami Khedira wa Real Madrid.
Unategemea nini zaidi?
Scolari alipaswa kucheza kama kibonde katika mechi
hii. Alipaswa kwanza kuichunga Ujerumani na si kuanza kuwashambulia kwa
kasi kama alivyofanya ndani ya dakika tano za mwanzo. Lilikuwa kosa
kubwa.
Kinachozungumzwa ni kwamba Scolari alikuwa
anatafuta bao la mapema na kisha timu yake irudi nyuma kwa ajili ya
kujihami na kucheza kwa umakini.
Bahati mbaya bao lenyewe la kwanza halikuangukia katika nyavu za Ujerumani, liliangukia katika nyavu zao.
Bao lenyewe halikuingia kwa staili ya kuonewa.
Ulikuwa mpira wa kona. Lakini baada ya hapo kikosi chake kikazidi
kufunguka kwa tamaa ya kusaka mabao ya kusawazisha.
Ni hapo ndipo kulionekana daraja kubwa eneo la
katikati la Brazil. Fernandinho na Gustavo wasingeweza kuifanya kazi hii
peke yao. Kulihitaji viungo wa kulibana eneo la katikati kwa ajili ya
kuwabana Wajerumani.
0 maoni:
Chapisha Maoni