Jumatatu, 17 Machi 2014

ZAMANI SIMBA , YANGA ILIKUWA GUMZO MTAANI, SASA YANGA VS AZAM FC WATU HAWALALI, KITAELEWEKA TAIFA KESHO KUTWA!!

KUELEKEA katika mechi ya keshokutwa ndani ya dimba la Taifa, jijini Dar es salaam baina ya mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Young Africans dhidi ya makamu bingwa kwa misimu miwili mfululizo, Azam fc wana Lambalamba mashabiki, viongozi na mabenchi ya ufundi yamepandwa na homa kali.
Azam fc waliopo kileleni wakiwa na pointi 43 wapo katika mipango kabambe ya kuhakikisha wanapata ushindi mbele ya Yanga inayotajwa kuwa na kikosi bora zaidi msimu huu.
Ni kweli Yanga msimu huu imesheheni majina ya wachezaji wenye mvuto zaidi nje ya uwanja, japokuwa ndani ya uwanja bado kuna matatizo ndani ya kikosi chao.
Ukitaja majina kama vile Emmanuel Anord Okwi, Hamis Friday Kiiza `Diego`, Didier Kavumbagu `Kavu`, Mrisho Khalfan Ngasa `Anko`, Simon Msuva , Said Bahanuzi, Jeryson John Tegete ambao huongoza safu ya ushambuliaji, hakika utahofia unapoingiza uwanjani kikosi chako cha bei  `chee` .
Pia ukija dimba la kati, unakutana na mafundi, Haruna Niyonzima `Fabregas`, Frank Domayo `Chumvi`, Athuman Idd `Chuji` , Hassan Dilunga na wengineo ambao hawana namba za kudumu katika kikosi cha kwanza.
Nayo safu ya ulinzi imesukwa kwa mabeki visiki wakiwemo Kelvin Patrick Yondan, Nadir Haroub `Canavaro`, Mbuyu Twite, Oscar Samwel Joshua, David Luhende na wengineo.
Ukiangalia tofauti ya majina baina ya Yanga na Azam fc, Wanajangwani ni chama kubwa zaidi kwa maana ya kuwa na mtaji mkubwa wa wanachama, mashabiki na hata ukongwe wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Ukija katika mipango, uwekezaji, hapo unaleta habari nyingine. Azam fc wameipiga bao Yanga kwa asilimia kubwa.
Wakati mashabiki wakisubiri mechi hiyo kwa hamu kubwa, tayari kikosi cha Yanga kimeingia chimbo maeneo ya Bagamoyo,  Mkoani Pwani kujiwinda na mechi hiyo ya kesho kutwa.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa kipa namba moja wa klabu hiyo aliyekosa mchezo wa jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar ulioishia kwa suluhu ya bila kufungana, Deogratius Munich `Dida` anaweza kurejea uwanjani kufuatia kuendelea vizuri baada ya kuumia katika mazoezi wiki iliyopita.
Naye Mrisho Ngasa aliyeumia katika mchezo wa machi 9 mjini Alexndria  dhidi ya Al Ahly ambapo Yanga walitolewa kwa penati 4-3 anaendelea vizuri ingawa bado hakuna uhakika kama anaweza kutumika mechi ijayo.
Hata kama `Dida` hatakuwepo katika mchezo wa kesho kutwa, bado nafasi yake itaweza kuzibwa na makipa waliopo, Juma Kaseja na Ally Mustapha `Bartez`.
Kaseja aliyesajiliwa maalum kwa mechi za kimataifa, alikosa mechi tatu za ligi ya mabingwa barani Afrika.
Alikosa mechi ya marudiano dhidi ya Komorozine mjini Moroni, na akakosa mechi mbili dhidi ya Al Ahly.
Lakini jumamosi kwenye mchezo wa Mtibwa Sugar, Kaseja alitumika na alionesha umahiri langoni, hivyo kama `Dida` hatocheza, lango la Yanga litakuwa katika mikono salama.
Nao vinara Azam fc wameshaingia kambini katika Hosteli zao zilizopo Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Ni mandhari nzuri kwao na masikani kwao, hivyo bila shaka wapo katika mipango madhubuti kuwaliza Yanga kwa mara nyingine tena ligi kuu soka Tanzania bara.
Yanga wanahitaji ushindi kwa nguvu zote ili wapunguze pengo la pointi dhidi ya Azam fc.
Mpaka sasa Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 39 baada ya kucheza mechi 18. 
Nyuma yao wapo Mbeya City wenye pointi 39 sawa na Wanjangwani, lakini utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa ndio unawafanya wagonga nyundo wa Mbeya kuwa nyuma.
Endapo Yanga watashinda mchezo wa jumatano, watafikisha pointi 42 nyuma ya Azam fc wenye pointi 43, hivyo pengo la pointi moja litawapa unafuu mkubwa.
Kama Azam fc watashinda, basi Yanga watazidi kuisoma namba. Endapo watatoka sare, basi Azam fc wataendelea kubarizi kileleni kwa raha zao.
Matokeo yoyote katika mchezo huo, hayatabadili nafasi mbili za juu.  Azam fc watabaki wa kwanza na Yanga watabaki wa pili, huku mechi za wikiendi zikisubiriwa ambapo Mbeya City watakupambana na JKT Ruvu, uwanja wa Chamazi.
Ugumu wa mchezo wa keshokutwa unachangiwa na mazingira mengi;
Moja; ubora wa Azam fc ambao mpaka sasa chini ya kocha wake Joseph Marius Omog hawajafungwa katika mechi 19 walizocheza.
Kutofungwa kwa mechi 19, kunakupa picha kuwa Azam fc wapo katika mikakati mizito ya kuchukua ubingwa.
Hawakufanya vizuri kombe la shirikisho mwaka huu, lakini mechi za mwisho za ligi kuu wamepata ushindi mkubwa sana katika uwanja wa Chamazi.
Wikiendi iliyopita waliwafunga Coastal Union 4-0, lakini kabla ya hapo nao Ashanti walikula 4-0.
Pia urejeo wa nahodha wao na mwenye bahati ya kuwatungua  Yanga, John Bocco `Adebayor` kumewaongezea nguvu zaidi Azam fc katika safu ya ushambuliaji ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiongozwa na Kipre Herman Tchetche na Mganda Brian Umony.
Siku za karibuni, Azam fc walionekana kuwa na tatizo nafasi ya beki wa kushoto kufuatia nyota wake, Samih Hajji Nuhu na Waziri Salum kuwa majeruhi kwa muda mrefu, lakini kwasasa pengo hilo  linaonekana kuzibwa vyema na beki aliyepandishwa kutoka kikosi cha pili, Gadiel Michael. 
Mechi ya mzunguko wa kwanza  Azam fc iliifunga Yanga SC mabao 3-2 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kabla ya mechi hiyo, timu hizo zilikutana katika mechi ya Ngao ya jamii ambapo Yanga waliilaza Azam fc bao 1-0.
Timu hizo zimekutana mara mbili msimu huu na kila moja kushinda na kufungwa, hivyo kwa haraka hakuna mbabe msimu huu, na Jumatano kila klabu itataka kuonesha kuwa ni bora zaidi.
Pili; Azam fc wanataka ubingwa wao wa kwanza msimu huu, huku Yanga wakihitaji pointi muhimu ili kupunguza pengo. Hivyo kutakuwa na upinzani mkubwa zaidi.
Tatu; ubora wa vikosi vyote. Yanga wana wachezaji wa gharama kubwa zaidi, lakini hawajafanikiwa kucheza kwa mafanikio ligi kuu soka Tanzania bara kama Azam fc.
Wao waliwahi kufungwa,  Azam fc hawajafungwa mpaka sasa. Hivyo utagundua kuwa timu hizi ni bora.
Kufungwa kwa Yanga hakumaanisha hawana timu bora, bado kikosi chao kinaonekana kuwa na makali. Mechi itakuwa ngumu zaidi.
Joto la mechi hii linazidi kupanda na ukipita mitaani unawasikia mashabiki wakizungumzia kipute hiki.
Nao viongozi wamesikika wakisema wapo katika mikakati mizito ya kuibuka na ushindi. 
Sina shaka kuwa mikakati hiyo inalenga kuziandaa timu zao kucheza mpira uwanjani.
Kama mikakati inayosemwa ni nje ya uwanja, sasa hapo kunakuwa na shaka juu ya ubora wa mechi yenyewe.
Makocha wa timu zote, Joseph Marius Omog wa Azam fc na Hans Van Der Pluijm wa Yanga wanaonekana kutuliza akili zao kuhakikisha wanawapa raha mashabiki wao.
Pluijm ana kazi kubwa ya kuhakikisha anapata ushindi ili kuwapa raha mashabiki wa Yanga ambao walifurika uwanja wa Jamhuri Morogoro, lakini waliambulia kuona timu yao inatoka suluhu.
Inafurahisha sana kuona mechi ya Azam fc dhidi ya Yanga inagusa hisia za mashabiki kwa kiasi kikubwa.
Miaka ya nyuma, mechi ya watani wa jadi pekee ndio ilionekana kuwa na mvuto kwa mashabiki.
Kila mtaa ukipita unasikia wakitambiana mno. Lakini sasa mambo yamebadilika kabisa.
Mechi ya Azam fc na Yanga inazungumzwa kila mtaa, pia mechi ya Yanga dhidi ya Mbeya City inaliteka jiji.
Pia ukija upande wa pili, Simba vs Azam fc, Simba vs Mbeya City, Simba vs Yanga zimekuwa mechi zenye mvuto mkubwa zaidi kwa mashabiki.
Hali hii imechangiwa na ujio wa Mbeya City na Azam fc kuzipatia changamoto Simba na Yanga.
Kimpira ni hatua nzuri. Unapokuwa na timu nyingi zenye ushindani na mvuto kwa mashabiki, unapata ligi bora kabisa.
Angalia mashabiki wa Mbeya City wanaokuja kuishangilia timu yao inapocheza uwanja wa Taifa, hakika unagundua kuwa kuna hatua soka la Tanzania linapiga.
Asante sana Azam fc na Mbeya City kwa kubadilisha utawala wa Simba na Yanga. Sasa wakongwe hawa huwa hawalali mnapokutana.
Ingekuwa vizuri zaidi ifike wakati tuwe na timu nyingi zaidi zenye mvuto kama Azam fc na Mbeya City ili tabia ya kutabiri matokeo na kuamini Simba na Yanga wanashinda ife kabisa.
Yanga na Azam fc onesheni ubora uwanjani ili muwape raha mashabiki wenu. 
Mpira unachezwa hadharani, na hauchezwi kwa siri. Tafuteni matokeo ndani ya uwanja na si nje ya uwanja.
Waamuzi chezesheni mpira kwa weledi. Sheria 17 zipo wazi, zifuateni bila kuwa na unazi wa timu.
Mkifanya kazi yenu kwa ufanisi, mtasababisha mpira bora kuonekana baina ya miamba hii miwili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top