Jumapili, 16 Machi 2014

           Anelka afukuzwa West Brom


By Israel Saria on March 15, 2014

West Bromwich Albion wamekata shauri la kumfukuza mchezaji mkongwe, Nicolas Anelka kwa utovu mkubwa wa nidhamu, baada ya mpachika mabao huyo kutangaza kwamba anaondoka Hawthorns.
West Brom walishamuonya Anelka, kumsimamisha kucheza mechi tano, ambapo Chama cha Soka (FA) kilimtoza faini ya £80,000 kwa kuonesha ishara ya ‘quenelle’ ambayo inatafsiriwa kuwa ni ya Kinazi.

Klabu imedhamiria kumfuta Anelka mwenye umri wa miaka 35 kwenye orodha ya wachezaji wake kwa kosa hilo na pia kwa kupayuka kwenye vyombo vya habari bila ruhusa, na wamempa notisi ya siku 14 kama kanuni zinavyotaka kabla ya kutengua mkataba wake.

Ishara hiyo hufanywa kwa kunyoosha mkono mmoja chini pamoja na vidole kando ya mguu wa upande huo huo, huku mkono mwingine ukiwekwa mbele kwenye bega la mkono ulioshushwa. Ilibuniwa na mwigizaji wa Ufaransa, anakotoka, Anelka, Dieudonne M’bala M’bala na inasemwa kwamba ni ishara ya kupinga mamlaka halali.

Anelka alitumia mtandao wa jamii kuandikia kwamba alikuwa anaondoka klabuni hapo mara moja kwa madai wameshindwa kufikia mwafaka na klabu, kwa kuwa amewekewa masharti ambayo hawezi kuyakubali na anataka kutunza heshima yake na hivyo amekatisha mkataba wake.

West Brom wanasema usitishaji wa mkataba anaodaiwa kufanya Anelka si wa kweli na ni batili kwa sababu haujafuata taratibu za kisheria zinazotakiwa. Masharti klabu iliyotoa ni kwa Anelka kuomba radhi klabu, washabiki, wadhamini na jamii nzima kwa athari za ishara aliyoitoa Desemba 28 mwaka jana na kasha akubali faini aliyotozwa.

Mkataba wa Anelka ambaye amechezea klabu nyingi ulikuwa umalizike mwishoni mwa msimu huu. Anelka ameichezea Timu ya Taifa ya Ufaransa tangu 1997 hadi 2010 na huko aliwahi kupata masahibu pia.
Katika ngazi ya klabu, Anelka alianzia kwenye timu za vijana za Trappes Saint-Quentin, Clairefontaine na Paris Saint-Germain.

Katika ngazi za wakubwa, kati ya 1996–1997 alikuwa Paris Saint-Germain, kisha akaenda Arsenal hadi 1999 alipohamia Real Madrid kabla ya kurudi Paris Saint-Germain mwaka 2000 lakini hakudumu kwani 2001 alipelekwa Liverpool kwa mkopo hadi 2002.

Anelka alijiunga na Manchester City 2002 alikocheza hadi 2005 akaenda Fenerbahçe kwa mwaka mmoja hadi 2006 alipohamia Bolton Wanderers akacheza hadi 2008 akasajiliwa Chelsea alikokaa hadi 2012 akaenda China kuchezea Shanghai Shenhua. Hakukaa sana kwa sababu mwaka uliofuata alikwenda Juventus kwa mkopo na mwaka jana akajiunga West Bromwich Albion ambao sasa wanamtema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top