RAGE ANA POINTI, SIMBA MAMBUMBUMBU
Ninaposikia kauli za viongozi wa vilabu vyetu hapa Tanzania, huwa najiuliza maswali mengi sana. Weekend hii umefanyika mkutano wa wanachama wa Simba Sports club katika bwalo la polisi pale Oyster Bay. Katika mkutano huo, mwenyekiti wa sasa wa klabu hiyo alitoa kauli zenye utata kidogo, miongoni mwa kauli zake ilikua hivi, “Simba oyeee…. Mimi sitagombea tena katika uchaguzi ujao, sina njaa, mimi sio masikini…. Hata mkinizomea nasemaje, sina njaa wala si masikini, msiwe kama mambumbumbu”.
Kauli
hizi za mwenyekiti wa klabu hii ya simba, zimeibua hoja kadhaa kichwani mwangu
ambazo nazitafakari katika makala hii.
Simba
Sports Club, timu iliyoanzishwa miaka ya 1930, na kuwa na wapenzi na wanachama
wanaokadiriwa kufikia milioni tano (5) kwa ujumla, hadi leo inafanyia mikutano
yake kwenye bwalo la polisi.
Simba
Sc, miongoni mwa timu zenye umri mkubwa hapa Tanzania, (inakadiriwa kuwa na
zaidi ya miaka 75), ina jengo kariakoo ambalo hata kupata eneo la kuegesha gari
ni taabu.
Hadi
leo, timu hii iliyowahi kufika makundi ya ligi ya mabingwa Afrika mwaka 2003,
haina mkataba na kampuni yoyote ya utengenezaji wa vifaa vya michezo, kama
Adidas au Nike wala kampuni yoyote kubwa, bali inategemea vifaa vya mchezo
kutoka kwa wadhamini wa ligi.
Hadi
leo, pesa za usajili wa wachezaji zinatoka mifukoni mwa watu wachache, na hata
mauzo ya wachezaji hao hurudi kwenye akaunti zao binafsi za benki, na hakuna
mwanachama mwenye uhalali wa kuhoji matumizi ya fedha hizo.
Hizi
ni baadhi ya hoja nilizonazo kichwani mwangu, ambazo zinaashiria ukweli wa
kauli ya mwenyekiti wa Simba, kwamba wanachama wake ni mambumbumbu. Sina maana
ya kumtukana wala kumkejeli mtu, ila nia yangu ni kuwafumbua macho wanachama wa
Simba, ili kama ni kufanya mabadiliko, basi wakati ndio huu wa kuondokana na
kauli za kudhalilishwa kutoka kwa viongozi wao.
Hivi
Simba Sc, ni kampuni, ama taasisi, ama biashara ya watu binafsi? Kwa utaratibu
uliopo kwasasa, inaashiria kwamba Simba Sc ni taasisi Fulani, inayopata udhamini
kutoka kwa wadhamini wa ligi na wadhamini wa timu, ambapo ndani yake inafanyika
biashara ya WATU Fulani wachache.
Mfano mzuri ni pale mwenyekiti wa club hii
alipoamua kufanya usajili wa mchezaji mmoja kutoka Zanzibar, na usajili ule
ulifanyikia sebuleni kwa mwenyekiti huyu, kwa kumkabidhi kitita cha fedha,
wakapiga picha, zikaenea mitandaoni. Endapo mchezaji huyu akiuzwa kwenda timu
nyingine kwa kitita kirefu zaidi, ni mwanachama gani
mwenye uhalali wa kuhoji matumizi ya pesa za mauzo yake? Maana hakuna mwanachama
anayejua pesa za manunuzi yake zilitoka wapi, ndio maana nimesema kwamba ni
biashara ya watu binafsi.
Kama
Simba Sc ingekua ni kampuni, leo hii mambo yangekua tofauti. Timu ingeweza
kujitegemea kiuchumi, ingekua na waajiriwa wa kudumu ambao wangeifanya timu hii
kuwa biashara ya kudumu kwa faida ya wanachama na wapenzi wote kwa ujumla na si
kwa watu wachache peke yake. Makampuni mbali mbali yangeweza kuwekeza kwenye
timu hii kwasababu imani ya matumizi ya pesa ingekuwepo.
Soka
ni mchezo wa burudani, na wala si siasa. Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na
washabiki wengi wa mpira wa miguu. Mchezo huu umekua ni miongoni mwa burudani
zinazopendwa na watanzania wengi nchini na nje ya nchi kwa kwa ujumla, miongoni
mwao ni wanasiasa, wasanii wa burudani mbali mbali pamoja na wafanyabiashara.
Miongoni mwa watu maarufu nchini ambao ni wapenzi wa timu ya Simba Sc ni pamoja
na wasanii wa muziki wakiwemo, Professor Jay, Mwana FA, Afande Sele na wengine
kibao. Kwa Wanasiasa kuna akina Mohammed Dewji, Zitto Kabwe, Professor Kapuya
na wengineo. Je, ni mara ngapi watu hawa maarufu nchini wenye uwezo mkubwa wa
ushawishi, wamewahi kuhudhuria mikutano ya wanachama? Kama hawajawahi
kuhudhuria, umewahi kujiuliza ni kwanini? Je, unadhani hawana kadi za
uanachama? Kama ni kweli hawana, jiulize ni kwanini?
Kaizer
Chiefs, Orlando Pirates, TP Mazembe, na Azam Fc, ni miongoni mwa timu chache
Afrika kuanzishwa baada ya club ya Simba Sc kuwepo, ambapo mafanikio ya timu
hizi ni ndoto kwa timu hii ya Simba. Sio kwasababu timu hizi zilianza zikiwa na
matajiri ama pesa lukuki, ila ni kwa sababu ni timu zilizoanzishwa kwa mipango
madhubuti ya kiutendaji.
Hadi
lini klabu kubwa kama Simba itaendelea kutawaliwa na watu kama akina Rage,
wenye kauli za udhalilishaji wa wanachama wake? Kuna wakati timu ilifanya
vibaya, mwenyekiti akapigiwa simu na radio moja kwa ajili ya mahojiano ili
kujua chanzo cha kufanya vibaya, jibu lake likawa kwamba yeye hachezi uwanjani,
hivyo hawezi kujua tatizo ni nini.
0 maoni:
Chapisha Maoni