Kwa Habari za Michezo
Logarusic aikochi Yanga mechi ya Al Ahly
KOCHA Mkuu wa Simba Mcroatia, Zdravko Logarusic, ameisaidia
Yanga mbinu za kuwafunga wapinzani wao Al Ahly watakaopambana nao Machi
Mosi katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika hatua ya awali ya michuano hiyo, Yanga iliitoa Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2.
Akizungumza na Mwanaspoti, Logarusic, alisema
wanachotakiwa kukifahamu Yanga na kocha wao, Hans Pluijim, ni kupanga
wachezaji wenye uwezo mkubwa bila ya kuangalia uzoefu, ukongwe wala
umaarufu.
Alisema kuwa Yanga wanatakiwa kucheza soka la kasi
linalotumiwa na klabu za Uarabuni kwa ajili ya kuendana na kasi ya Ahly
ndani ya uwanja na si kucheza taratibu kama wanavyofanya katika mechi
za Ligi Kuu Bara.
Aliongeza kuwa wanapaswa kutumia akili nyingi na
kucheza kwa tahadhari kubwa na kwamba viungo wao hawatakiwi kuwapa
nafasi wachezaji wa Ahly kumiliki mpira muda mrefu kwani alisema Ahly
huanzisha mashambulizi yao katikati na si pembeni.
“Wanatakiwa kucheza kwa kutumia akili nyingi,
wasiwape nafasi viungo wa Ahly kumiliki mpira muda mrefu, wakiwaachia
basi watapoteza mechi zote mbili, ya nyumbani na ugenini,” alisema.
“Yanga wanatakiwa kujaza viungo wengi kwa ajili ya
kuizuia safu ya kiungo ya wapinzani wao kutawala mpira, ninauamini
uwezo wa kufundisha wa kocha wa Yanga katika kutengeneza timu.”
Pluijm kwa upande wake alisema: “Nawaandaa
wachezaji wangu katika kucheza kwa kasi, nguvu na uwezo wa kufikiri. Pia
namna ya kufunga mabao wakiwa karibu kabisa na lango.
Ahly yashinda, Polisi wavamiwa
Polisi 25 wamejeruhiwa vibaya baada ya kuibuka
mapambano kati yao na mashabiki wa Al Ahly muda mfupi baada ya mchezo wa
Super Cup ulioikutanisha timu hiyo na Sfaxien ya Tunisia juzi Alhamisi
na Ahly kushinda mabao 3-2.
Mchezo huo uliikutanisha Al Ahly bingwa wa Ligi ya
Mabingwa Afrika na Sfaxien ambayo ni bingwa wa Kombe la Shirikisho,
ulichezwa kwenye Uwanja wa Cairo na kuruhusiwa na Fifa na Serikali
kuingiza mashabiki 30,000 tu ikiwa ni ruhusa maalumu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Misri, mapambano hayo ya polisi na mashabiki, yalitokea sekunde
chache baada ya mchezo huo kumalizika ambapo mashabiki wa Al Ahly
walivamia uwanja na kuanza kurusha vitu mbalimbali.
Okwi akabidhiwa vita ya Azam na Yanga
KWA idhini ya Fifa, Yanga itamrejesha kwa mara ya kwanza
uwanjani straika wake, Emmanuel Okwi ambaye usajili wake ulikuwa na
utata.
Benchi la ufundi limempa kazi moja tu kuipiga Ruvu
Shooting na kupunguza nyodo za Azam inayopepea kileleni kwenye msimamo
wa Ligi Kuu Bara.
Azam chini ya Kocha wake, Mcameroon, Joseph Omog
ilikuwa na malengo mawili msimu huu, kucheza hatua ya makundi ya Kombe
la Shirikisho na kutwaa ubingwa wa Bara. Lakini baada ya kuchemsha na
kutolewa na Ferroviario ya Msumbiji, Straika wa Azam, Kipre Tchetche
ameliambia Mwanaspoti kwamba sasa hasira zao ni kwenye Ligi Kuu na
watapambana kiume wakianza dhidi ya Prisons kesho Jumapili kwenye Uwanja
wa Chamazi.
Mechi ya Yanga leo Jumamosi ni muhimu kwao kusaka
pointi za kuongoza lakini mashabiki wamepania kuona vitu vya Okwi
aliyekuwa amezuiwa kucheza na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF)
lililokuwa likitaka muongozo wa Fifa ambao waliwajibu kuwa Okwi ni
halali.
Ruvu Shooting imembeza Okwi na imewapa kazi mabeki
wake wawili, Mbonosi Mangasini na Shaaban Sunza ‘Chogo’ wahakikishe
kwamba straika huyo hana madhara.
Mkenya Tom Olaba ambaye ni kocha wa Ruvu alisema:
“Eti kila mtu Okwi, Okwi kwani huyo Okwi ni nani. Hivi huyo ni mtu
spesho sana, Okwi, Okwi anaweza kucheza na wachezaji 11 wa Ruvu,
simhofii hata kidogo, nitakachokifanya ni kucheza na timu nzima na si
yeye mmoja.”
Olaba hawajui wala hajawaona Yanga ila
atakachokifanya, ndani ya dakika 15 za mwanzo ni kuwasoma na kuwadhibiti
ingawa kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa aliifundisha Ruvu
mzunguko wa kwanza hivyo anajua kiufundi uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm ambaye
atawakosa, Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ mwenye kadi tatu za
njano, Hussein Javu na Reliants Lusajo ambao ni majeruhi alisema: Tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda, timu ipo vizuri.
Coastal Union vs Mbeya City
Mbeya City itatokea Mombasa ilikokuwa imeweka
kambi ya muda kuja Tanga kuikabili Coastal Union ambayo kiwango chao
hakijauridhisha uongozi kutokana na matokeo hafifu ambayo hayaendani na
kambi waliyoweka Oman.
Noah tano za madiwani wa Jiji la Mbeya na mabasi
matatu ya mashabiki yaliingia Tanga jana Ijumaa usiku kuisapoti timu yao
katika mechi hiyo.
Azam inaongoza ligi hiyo na pointi 36, Yanga ni ya
pili ina 35, pointi sawa na Mbeya City inayoshika nafasi ya tatu,
wakati Simba ni ya nne ina pointi 32.
Logarusic: Nipo tayari kujiuzulu
KOCHA wa Simba Mcroatia, Zdravko Logarusic (52) amesema yupo tayari kubwaga manyanga endapo uongozi hautaridhika na mwenendo wa timu aliyoanza kuinoa Desemba mwaka jana.
Simba ilishinda mechi dhidi ya Rhino Rangers na JKT Oljoro huku ikitoka sare na Mtibwa Sugar na Mbeya City na kufungwa na Mgambo JKT 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, katika Makao Makuu ya Klabu ya Simba, Msimbazi, Kariakoo, Dar es Salaam jana Ijumaa, Loga alisema: “Mimi ni kocha mzoefu na nimewahi kufundisha baadhi za timu za Afrika hivyo kama Simba wataona mwenendo wa timu si mzuri, nitakuwa tayari kuondoka mwenyewe bila ya kufukuzwa na viongozi.”
“Mfano niliondoka Gor Mahia ya Kenya bila kufukuzwa wakati timu ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa, ni jambo la kushangaza ila kama kocha lazima ukubali kubeba mzigo,” alisema.
Logarusic amekifanyia mabadiliko kikosi chake kabla ya mchezo wa kesho Jumapili dhidi ya JKT Ruvu, katika mabadiliko hayo jeshi hilo linaundwa na viungo wakabaji saba.
Loga amekuwa akiwatumia kiungo Henry Joseph kucheza kama beki wa kushoto, William Lucian ‘Gallas’ akiwa kulia wakirahisisha majukumu ya ukabaji wakisaidiana na mabeki wa kati Donald Mosoti na Joseph Owino huku katika kiungo kukiwa na Jonas Mkude, Said Ndemla, Ramadhan Singano ‘Messi’, Haruna Chanongo na Amri Kiemba.
Alisema; “Siku zote hatumpangi mchezaji kwa kuangalia anacheza namba gani, tunachofanya tunampanga mchezaji kwa kumpa majukumu yake anayotakiwa kuyatekeleza uwanjani.
Chuji, Okwi kuibeba Yanga Misri
KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima anaamini kurejea kikosini kwa
kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ na straika Emmanuel Okwi kumeiongezea nguvu
timu yao na morali ya kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Al Ahly.
Yanga itacheza mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi
ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri Jumamosi ya Machi Mosi
mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Chuji hakuwepo katika kikosi cha Yanga
kilichocheza mechi ya awali hapa nchini dhidi ya Komorozine kutokana na
kutumikia adhabu ya kadi nyekundu lakini alicheza pambano la marudiano
mjini Mitsamiouli, Comoro. Okwi alikuwa na matatizo ya usajili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Niyonzima alisema Chuji
na Okwi ni wachezaji wenye uzoefu na mechi za kimataifa, hivyo
wataisaidia Yanga kufanya vizuri mbele ya Al Ahly ambao ni mabingwa
watetezi wa michuano hiyo.
“Naamini Chuji na Okwi watatusaidia katika mechi
dhidi ya Al Ahly, hii si mechi ndogo hivyo inahitaji wachezaji wenye
uzoefu na uwezo wa hali ya juu, nadhani kocha atajua nini cha kufanya
ili tuwe nao kikosini japokuwa yeye ndiye anaamua nani acheze.
“Si kwamba wachezaji waliobaki hawana mchango
katika Yanga, lakini kiuhalisia Chuji na Okwi wana mchango wao katika
timu kama ilivyo kwa wachezaji wengine,” alisema Niyonzima.
Baada ya mchezo wa kwanza nchini, timu hizo
zitarudiana baada ya siku saba nchini Misri ambapo idadi ya mashabiki
maalumu ndiyo itakayoruhusiwa kuingia uwanjani kutazama mechi hiyo.
Yanga imeingia kambini Bagamoyo katikati ya wiki
hii siku chache baada ya kurejea nchini kutoka Comoro ilipocheza na
Komorozine na kuitoa katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao 12-2.
0 maoni:
Chapisha Maoni