MSIMU wa shida Manchester United. Hicho ndicho unachoweza kusema baada ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England kuporomoka hadi nafasi ya nane kwenye msimamo kutokana na sare ya mabao 2-2 waliyoipata jana Jumapili dhidi ya Tottenham Hotspurs kwenye Uwanja wa White Hart Lane.
Mabao mawili ya straika, Wayne Rooney, yalishindwa kuinusuru timu hiyo walau kupanda nafasi za juu kwenye msimamo huo baada ya sare hiyo kuwafanya kufikisha pointi 22 baada ya kucheza mechi 13. Hata hivyo, kikosi hicho kinachonolewa na David Moyes, kinaweza kushukuru kuambulia pointi hiyo moja ya ugenini baada ya mabao yake hayo iliyoyapata kwa kusawazisha.
Tottenham ilitangulia kwa bao la mpira wa adhabu uliopigwa na Kyle Walker kabla ya Sandro kufunga kwa shuti kali akiwa umbali wa mita 25.
Rooney alifunga bao lake la kwanza kwenye mchezo huo akitumia makosa ya beki Walker aliyeshindwa kuokoa krosi ya Phil Jones, wakati lile la pili lilitokana na mkwaju wa penalti iliyosababishwa na kipa Hugo Lloris kumwaangusha Danny Welbeck kwenye eneo la hatari.
0 maoni:
Chapisha Maoni