• Adai
wanakwenda ofisini kwake kuombaomba

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda
amesema kuwa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili wabunge
wanapomaliza vipindi vyao, ofisi yake imelazimika kutoa mafunzo ya
ujasiriamali ili waweze kumudu maisha.
Makinda alitoa kauli hiyo jana
wakati akibadilishana mawazo na Spika wa Bunge la Uswisi, Maya Graf ambaye
yupo nchini kwa mapumziko mafupi na familia yake.
Alisema kuwa kwa kipindi alichokaa
katika kiti cha uspika, amebaini matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wabunge
waliostaafu.
Makinda alisema kuwa wabunge wengi
wamekuwa wakiathirika kiuchumi pindi wanapotoka katika nafasi hiyo, hivyo
mafunzo yatawawezesha kuwa na shughuli za kufanya, na kwamba yatatolewa kwa
wabunge wote.
Alisema kuwa ni muhimu wabunge
wakaichukulia siasa kuwa sio kazi ya kudumu ili wanaposhindwa kuchaguliwa,
wafanye shughuli nyingine za kuwaingizia kipato.
“Hata ukiangalia magomvi
yanayotokea wakati wa uchaguzi, wengi wasiokubali matokeo ni wale ambao
hawana shughuli za kufanya,” alisema.
Spika Makinda alisema kuwa kwa
wabunge ambao wana shughuli za kufanya, kwao ubunge unakuwa sio tatizo kwa
kuwa wana uwezo wa kuendesha maisha yao.
Alisema tangu ashike nafasi hiyo,
wabunge wengi walioshindwa uchaguzi wamekuwa wakifika ofisini kwake na kuomba
msaada wa kifedha wakati ofisi hiyo haina fungu la wastaafu hao.
“Kuna siku nilikuwa ofisini
walikuja wabunge wastaafu zaidi ya watano wakiomba msaada, ikanilazimu nitoe
akiba yangu nikawasaidia baadhi, lakini wale ambao hawakupata chochote
walinung’unika sana,” alisema.
Makinda alisema kuwa kabla ya
mwaka 1995, Bunge liliweka utaratibu wa pensheni kwa wabunge wastaafu, lakini
uliondolewa na anachopata sasa mbunge ni posho ya kumaliza vipindi vyake vya
ubunge.
Alisema kuwa na hiyo inatokana na
mishahara midogo wanayopata wabunge ukilinganisha na mabunge mengine.
“Hata ukiangalia fedha unayopata,
unatakiwa kuigawa na nyingine kupeleka jimboni, nyingine wengine wanatumia
wakati wa uchaguzi jambo linalofanya mbunge akikosa kuchaguliwa akose la
kufanya,” alisema.
Naye Graf, alisema kuwa wabunge wa
nchi yao hawana shida pale wanaposhindwa kuchaguliwa kwa kuwa wana uwezo wa
kupata kazi nyingine, na ajira sio tatizo.
|
0 maoni:
Chapisha Maoni