Jumatano, 23 Oktoba 2013

Babu ashinda mamilioni ya kamari mjukuu wake kupangwa





BABU mwenye furaha wa kinda wa Liverpool, Harry Wilson,   amefanikiwa kuibuka na kitita cha Pauni 125,000 baada ya kutabiri kuwa siku moja mjukuu wake angeichezea timu ya taifa ya Wales wakati huo kinda huyo alipokuwa na umri wa miezi 18 tu.
Wilson ambaye yupo katika timu ya vijana ya Liverpool, aliingia katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia baina ya Wales na Ubelgiji Jumanne ya wiki iliyopita huku akiwa na umri wa miaka 16 na siku 207.
Peter Edwards, 62, aliingia katika jumba la kamari la William Hill eneo la Wrexham mwaka 2000 na kuweka kiasi cha Pauni 50 akitabiri kwamba siku moja mjukuu wake atakipiga katika timu ya taifa ya Wales.

Lakini kocha, Chris Coleman wa Wales, alimwita mchezaji huyo kikosini kwa mara ya kwanza baada ya kuibuka nyota katika timu ya vijana ya Wales na Jumanne iliyopita usiku alimwingiza uwanjani akitokea katika benchi. Jambo hilo ndilo limempatia babu wa kinda huyo mamilioni ya pesa.

Kutokana na pesa hizo pia, babu huyo ameamua kustaafu kazi zake za kuendesha pikipiki eneo la Buckingham alikokuwa akifuatilia mechi hiyo kwa karibu akitumia iPad yake.
Kwa mwaka mzima, Edwards ambaye anafanya kazi katika eneo la Corwen, Clwyd, kaskazini mwa

Wales alilazimika kuhamia Buckingham kikazi, lakini baada ya mjukuu wake kumpatia noti hizo sasa anarejea kwa mkewe Dorothy, 58 kwa ajili ya kupumzika.
“Mke wangu amefurahi sana. Mimi ninastaafu moja kwa moja. Nilimwambia Meneja wangu jana (Jumatatu kabla ya mechi) kama Harry akicheza basi siji kazini tena,” alisema Edwards akizungumzia kutoka nyumbani kwake.

“Nimestaafu mwaka mmoja kabla ya wakati. Nimerudi zangu nyumbani na sitarudi tena kazini (Buckingham). Sio mbaya kwa pesa nilizopata.”
Edwards anakiri kwamba aliweka pesa zake baada ya kugundua kwamba mjukuu wake, Harry, alionekana kupenda kucheza soka hata alipokuwa bado mtoto mchanga.

“Alipendelea kuukimbiza mpira kwa mikono wakati akitambaa kabla hata hajaanza kutembea. Hilo ndilo lilinipa wazo la kwenda kucheza kamari. Nilikuwa na matumaini kwamba siku moja mambo yangeenda sawa,” anaongeza Edwards.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top