Baada ya Shirika la Simu za Apple kukataa kushirikiana na Idara ya Polisi ya Upelelezi Marekani FBI katika kuifungua simu aina ya iPhone iliyotumiwa na mtu anayedaiwa kutekeleza mauaji San Bernardino, California mwaka jana, shirika moja la Kizayuni limepewa jukumu la kuifungua simu hiyo.
FBI imesema kuwa imepata njia ya kuifungua simu hiyo ambayo imefungwa na nywila ya siri. Shirika la mitandao ya intaneti la Cellebrite ambalo huunda programu za kiusalama za simu za mkononi, limesema linashirikiana na FBI kuidukua simu hiyo.
Shirika la Cellebrite ambalo ni tawi la shirika la Sun Corp la Japan limesema linaweza kuunda programu mpya itakayowezesha kufunguliwa simu hiyo ya iPhone na hivyo kuhitimisha mvutano baina ya FBI na Apple.
FBI imekuwa ikilishinikiza shirika la Apple kufungua simu ya iPhone iliyokuwa ikitumiwa na mmoja kati ya waliotekeleza mauaji ya San Bernardino lakini Apple imekataa kufanya hivyo kwani huo utakuwa mwanzo wa kudukuliwa taarifa katika simu za watumiaji wa simu za iPhone.
Shirika la Apple limeishtaki FBI katika mahakama nchini Marekani lakini kesi hiyo ambayo ilikuwa imepangwa kusikilizwa Jumamosi iliyopita imeakhirishwa kufuatia ombi la serikali ya Marekani. Watetezi wa haki za binadamu wamelalamikia hatua ya kuakhirishwa kesi hiyo. Wiki mbili zilizopita pia, Rais Obama wa Marekani alisema anapinga kuundwa simu za mkononi ambazo maafisa wa serikali hawataweza kupata maelezo yaliyo ndani kila wanapotaka. Kwa msingi huo Obama aliiunga mkono FBI katika malumbano yake na shirika la Apple.
Serikali ya Marekani inasisitiza ulazima wa mashirika ya ujasusi nchini humo kuwa na uwezo wa kudukua simu za raia wa nchi hiyo. Mashirika mengine ya teknolojia za habari na mawasiliano kama vile Google, Facebook na Microsoft kidhahiri yametangaza kuunga mkono msimamo wa Apple. Kwa muda mrefu sasa mashirika ya teknolojia za habari na mawasiliano yamekuwa yakikakamikia hatua ya taasisi za usalama nchini humo kufanya ujasusi kuhusu watumizi wa simu za mkononi na intaneti. Lakini serikali ya Marekani inaamini kuwa makundi ya kigaidi kama ISIS au Daesh yamekuwa yakitumia huduma za simu za mkononi na intaneti kuwasiliana na kuandaa hujuma na mashambulizi.
Kwa vyovyote vile, malumbano baina ya FBI na Apple yanaweza kuwa na taathira katika uwezo wa mashirika ya usalama na ujasusi ya Marekani kuwa na uwezo wa kupata kirahisi maelezo ya intaneti na simu za mkononi ya watumiaji. Kuingia Wazayuni katika mgogoro huo kutaufanya upanuke zaidi. Ni wazi kuwa Wazayuni sawa na serikali ya Marekani, wanataka kukiuka faragha na kuwafanyia ujasusi watumiaji wa simu za mkononi na intaneti.
Pamoja na hayo, kuna weledi wa mambo wanaoamini kuwa, mgogoro baina ya Apple na FBI ni wa kidhahiri tu kwa ajili ya kupotosha fikra za waliowengi duniani kwani ukweli wa mambo ni kuwa, mashirika ya usalama ya Marekani kwa muda mrefu yamekuwa na uwezo wa kudukua na kupata habari zote za siri katika simu za mkononi za raia wa Marekani na hata wa maeneo mengine duniani.
0 maoni:
Chapisha Maoni