Jumanne, 29 Machi 2016

JUMA ABDUL MNYAMANI; SIMBA HAWANA UBAVU WA KUPORA UBINGWA YANGA


BAADA ya kustaafu kwa Nsajigwa Shadrack Mwandemele, klabu ya Yanga inaelekea kupata suluhisho la beki ya kulia, kufuatia kuja vizuri kwa Juma Abdul Jaffar Mnyamani.
Ni rahisi kusema Juma Abdul kwa sasa iwapo utaulizwa beki mbili wa Yanga nani – na hiyo tu ni kwa sababu tayari kijana huyo amejihakikishia kuwa mmiliki wa nafasi hiyo.
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE wiki hii imefanya mahojiano na mchezaji huyo ambaye anaelekea kumaliza Mkataba wake Jangwani mwishoni mwa msimu.
Juma Abdul amezungumzia mengi, ikiwemo mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly, akisema kwamba Yanga ya sasa ni bora zaidi tofauti ya miaka miwili iliyopita. Endelea.
Juma Abdul Jaffar Mnyamani, beki tegemeo wa kulia Yanga
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Habari za leo beki 
JUMA ABDUL: Nzuri tu kaka, mambo vipi
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Salama, hongera naona uko katika msimu mwingine mzuri Yanga
JUMA ABDUL: Ndiyo, tunashukuru tunaendelea vizuri
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Lakini nasikia Mkataba wako unaelekea ukingoni Yanga
JUMA ABDUL: Ni kweli, lakini nimekwishaongea nao, na tumefikia makubaliano bado kusaini tu Mkataba mpya.
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Lakini kulikuwa kuna habari za kwenda Qatar, imefikia wapi? 
JUMA ABDUL: Kulikuwa kuna mchongo wa Qatar, kuna wakala nilizungumza naye, lakini kwa bahati mbaya sijui ilikuwaje, mawasiliano yakapotea. Nikawa simpati tu katika simu yake, mwishoni nikaamua kuachana naye
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Pole sana, kama riziki yako ipo, iko siku itakurudia
JUMA ABDUL: Inshaallah bro, nami naamini hivyo hivyo
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Unaizungumziaje miaka yako minne Yanga?
JUMA ABDUL: Miaka miwili ya kwanza haikuwa mizuri sana, kutokana na kuandamwa na maumivu, lakini namshukuru Mungu miaka miwili ya pili nimeanza kufanya vizuri na sasa naelekea kusaini Mkataba mpya
Juma Abdul (kushoto) akimfukuza winga wa Azam FC, Farid Mussa

BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Changamoto kubwa unayokutana nayo Yanga ni ipi?
JUMA ABDUL: Yanga ni timu kubwa, ina wachezaji wengi wazuri, na wanacheza namba tofauti, kwa hiyo ushindani wa namba ni mkubwa, hivyo lazima niongeze bidii ili niwe fiti kila siku.
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Umewezaje kumpora namba Mbuyu Twite?
JUMA ABDUL: Sijampora namba Mbuyu, yule hakuletwa Yanga kama beki wa kulia, sema ilibidi awe anacheza beki ya kulia kwa sababu wakati ule mimi kiwango kilikuwa bado kipo chini. Ila baada ya mimi kupandisha kiwango, yeye akarudishwa katika nafasi yake na mimi nikaanza kucheza nafasi yangu
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Unayazungumziaje maisha ya Yanga kwa ujumla
JUMA ABDUL: Yanga raha sana, hakuna kitu kizuri kama wachezaji kuwa kitu kimoja, Yanga kuna umoja kuanzia kwa makocha na wachezaji, tunapendana na tuna umoja ambao unatuunganisha hadi na mashabiki wetu
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Unaizungumziaje Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, naona Simba wanaelekea kuwapokonya ubingwa?
JUMA ABDUL: Wale hawawezi, watasubiri sana Watakuwa wanaongoza hivyo hivyo wakati wenye ligi hatupo, tukirudi mechi mbili tu tunawapoteza tena
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Na Azam je?
JUMA ABDUL: Azam kweli ni washindani wetu, lakini na wao tutawapoteza tu mbele mbele kidogo
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Mmezitoa Cercle de Joachim (ya Mauritius ) na APR (ya Rwanda), katika Ligi ya Mabingwa, sasa mnakwenda kukutana na Al Ahly (ya Misri), unasemaje?
Juma Abdul (kushoto) ni mtaalamu wa kupiga mipira ya kichwa pia

JUMA ABDUL: Tunakwenda kukutana na timu ambayo ni kubwa, inafahamika, sisi kama Yanga tu mwaka juzi tumecheza nayo ikatutoa kwa taabu kwa penalti baada ya kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake. Miaka miwili baadaye tunakutana nayo tena, wazi itakuwa mechi ya ushindani sana.
Unaweza kuona Yanga vimeongezeka vitu kutoka Yanga ile iliyocheza na Al Ahly mara ya mwisho, hatujui na upande wao, ila nadhani sasa ndiyo tutawatazama ili kuwajua wakoje. Amini zitakuwa mechi mbili za kufa mtu, Dar es Salaam na Cairo. 
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Umoja wa Yanga dhamira yenu nini mwaka huu? 
JUMA ABDUL: Tunataka kuitoa Al Ahly ili tuingie hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa tukiamini mashindano haya yatatutangaza wachezaji na kujiuza pia. Na hata Yanga kama timu itapata heshima
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Upo timu ya taifa, lakini bado hujawa na namba kikosi cha kwanza, unadhani kwa nini?
JUMA ABDUL: Taifa Stars kuna Shomary Kapombe anafanya vizuri kuanzia klabu yake (Azam FC) hadi timu ya taifa. Nahitaji kuongeza bidii, ili siku moja ikitokea nikapewa nafasi nami nifanye vizuri niaminike
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Tupe histora yako kwa ufupi;
JUMA ABDUL: Mimi ninaitwa Juma Abdul Jaffar Mnyamani, nimezaliwa Novemba 10, mwaka 1992
Mwananyamala, Dar es Salaam. Elimu ya Msingi nimesoma Morogoro, shule inaitwa Mji Mkuu.
Nikiwa darasa la saba, nilichaguliwa timu ya mkoa ya shule za Morogoro, tukacheza mashindano ya Kombe la (Iddi) Kipingu (Luteni Mstaafu). Katika mashindano yale nikabahatika kuchaguliwa kwenda kujiunga na sekondari ya Makongo wakati huo Mkuu wake alikuwa Kipingu. Nilisoma pale hadi Kidato cha Nne nikaamua kuelekeza nguvu zangu kwenye soka.
Nikaenda Mwanza kujiunga na timu moja inaitwa Mwanza United ilikuwa Daraja la Kwanza mwaka 2009, baada ya msimu mmoja, Toto Africans ya Ligi Kuu ikaniona na kunisajili mwaka 2010.
Baada ya msimu mmoja tu Toto, timu kibao zikanifuata, lakini nikavutiwa na ofa ya Mtibwa Sugar ambayo nilijiunga nayo mwaka 2011. Nilicheza Mtibwa hadi mwaka 2013 nikaja Yanga.
Juma Abdul (wa pili kushsoto) mstari wa mbele katika kikosi cha Yanga cha sasa

BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Unaweza kutuelezea maisha yako binfasi kidogo, una mke au mchumba? 
JUMA ABDUL: Mke sina, ila nina mtoto mmoja anaitwa Mudrik ana mwaka mmoja. Mama yake bado hatujaoana, mimi ninaishi mwenyewe tu peke yangu nimepanga Sinza, lakini nyumbani kwetu Tandale
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Hujafanikiwa kuwa na nyumba yako tu mchezaji wa klabu kubwa kama wewe unayelipwa vizuri?
JUMA ABDUL: Ndiyo nipo katika hatua za mwishoni za ujenzi wa nyumba yangu eneo la Kongowe, na pia nina mpango wa kujenga nyumba nyingine Mbezi Mungu akijaalia, ambako tayari nina kiwanja 
BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE: Tunashukuru na tunakutakutakia maandalizi mazuri ya mechi zijazo
JUMA ABDUL: Asante, nawe pia nakutakia kazi njema
Juma Abdul (kushoto) akiwa na Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: JUMA ABDUL MNYAMANI; SIMBA HAWANA UBAVU WA KUPORA UBINGWA YANGA Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top