Jumatatu, 22 Juni 2015

VYETI VYAMNYIMA ULAJI MATOLA TAIFA STARS, MOROCCO ‘ALA SHAVU’ KIULAINI

Suleiman Matola (kulia) akiwa na kocha wa zamani wa Simba SC, Mserbia Goran Kopunovic
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KURUGENZI ya Ufundi ilimpendekeza Kocha Msaidizi wa Simba SC, Suleiman Matola awe Msaidizi wa Charles Boniface Mkwasa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars- lakini Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemkataa kwa sababu hana sifa.
Kamati ya Utendaji imemteua Hemed Morocco kuwa Msaidizi wa Mkwasa kwa sababu Matola hana vyeti vya kumpa sifa ya kupewa nafasi hiyo.
Na wakati Morocco anateuliwa, Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliwaambia Wajumbe kwamba itasaidia benchi la Ufundi la Taifa Stars kuwa na sura ya kitaifa, kwa sababu Mkwasa ni wa Bara na Morocco wa visiwani. 
Kamati ya Utendaji ya TFF Jumamosi ilimfuta kazi aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Mholanzi, Mart Nooij na habari zinasema Mkwasa atashika timu kwa muda. 
Kamati ya Utendaji ya TFF ililazimika kufanya kikao cha dharula baada ya Stars kufungwa mabao 3-0 na Uganda usiku wa juzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika mchezo wa kwanza Raundi ya kwanza kufuzu CHAN 2016. 
TFF italazimika kumlipa Nooij dola za Kimarekani zisizopungua 125, 000 (Sh. Milioni 250,000) kwa kumvunjia Mkataba, ambao ni mishahara yake ya miezi 10, kwa sababu kwa mwezi alikuwa analipwa dola 12,500 (Sh. Milioni 25).
Mabao mawili ya mshambuliaji Erisa Sekisambu na lingine la Farouk Miya yanahitimisha historia ya kocha huyo Mholanzi Tanzania. 
Mtihani wa kwanza wa Mkwasa na Morocco ni kujaribu kushinda mabao 4-0 ugenini wiki mbili zijazo dhidi ya Uganda mjini Kampala, ili kusonga mbele CHAN. 
Matokeo ya juzi yaliwakosesha wachezaji wa Taifa Stars donge nono la Sh. Milioni 1 kila mmoja ahadi iliyotolewa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi jana.
Mchezo wa Jumamosi ulikuwa wa tano mfululizo, Taifa Stars inafungwa chini ya Nooij aliyerithi mikoba ya Mdenmark Kim Poulsen Aprili mwaka jana na kwa ujumla timu hiyo imecheza mechi tisa bila ya ushindi chini ya Mholanzi huyo. 
Kwa ujumla, Nooij ameiongoza Stars katka mechi 18 tangu arithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen Aprili mwaka jana, kati ya hizo ameshinda tatu tu, sare sita na kufungwa tisa- akifunga mabao 17 na kufungwa 28.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: VYETI VYAMNYIMA ULAJI MATOLA TAIFA STARS, MOROCCO ‘ALA SHAVU’ KIULAINI Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top