Netanyahu atakiwa asiende kuhutubia Kongresi
Wazayuni walio wengi wanamtaka Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala
wa Kizayuni wa Israel afute mpango wake wa kutaka kuhutubia Kongresi ya
Marekani mwezi ujao. Uchunguzi wa maoni uliofanyika huko Israel
unaonyesha kuwa, Wazayuni walio wengi wanaamini kwamba mpango huo wa
Netanyahu utasababisha kutokea mpasuko na mivutano zaidi kati ya Tel
Aviv na Washington. John Boehner Spika wa Bunge la Marekani amemualika
Netanyahu ili akahutubie kwenye baraza hilo mwezi ujao, hotuba ambayo
inatarajiwa kujikita zaidi katika masuala ya kuwekwa vikwazo zaidi vya
Wamagharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hayo yanajiri katika
hali ambayo, Rais Barack Obama amepinga vikali mpango wa kuwekwa vikwazo
zaidi dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, kuchukuliwa hatua hiyo
kutasababisha kuvurugika mwenendo wa mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran
na kundi la 5+1. Obama pia amesema kuwa, hana mpango wa kukutana na
Netanyahu atakapoizuru Marekani. Uchunguzi huo wa maoni unaonyesha kuwa,
asilimia 62 ya Wazayuni wanaamini kwamba, hotuba ya Benjamin Netanyahu
haitaweza kuathiri makubaliano yajayo ya nyuklia kati ya Iran na nchi
sita zenye nguvu duniani ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Russia, China,
Marekani na Ujerumani.
0 maoni:
Chapisha Maoni