Jumatatu, 16 Februari 2015

Kutumiwa watoto vitani katika nchi zaidi ya 20 duniani.

Ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuwa, watoto wadogo wamekuwa wakitumiwa kama askari vitani katika nchi zaidi ya 20 duniani. UNICEF imetahadharisha katika ripoti yake hiyo kwamba, kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu duniani kunakosababishwa na kuongezeka vita katika maeneo mbalimbali kumewaweka watoto katika tishio kubwa la kutumiwa na makundi ya wanamgambo kama askari vitani. Ripoti hiyo inabainisha kwamba, vita vya Iraq, Syria, Afghanistan na katika nchi kadhaa za Kiafrika vimepelekea makumi ya maelfu ya watoto kukabiliwa na madhara makubwa. Ripoti hiyo inaonesha kuwa, watoto wenye umri wa miaka minane wamekuwa wakilazimika kushiriki vitani na hata kutekeleza operesheni za kujitolea muhanga.
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya watoto na mwakilishi maalumu wa UN katika mgogoro wa kijeshi wameandaa ripoti ya pamoja ambayo inaonyesha kuwa, makundi 57 ya wanamgambo na ya wabeba silaha katika nchi zaidi ya 20 duniani yamekuwa yakiwatumia watoto katika masuala ya vita. Akthari ya watoto hao ima wamekuwa wakishuhudia jinai zisizo na maelezo au wamekuwa wakilazimika kushiriki katika jinai za kivita, imebainisha ripoti ya UNICEF. Aidha ripoti hiyo inabainisha kwamba, sio watoto wa kiume tu ambao wamekuwa waathirika wa vita bali hata mabinti wadogo nao wamekuwa wakitumiwa vibaya na makundi ya wabeba silaha ambapo baadhi yao wamekuwa wakifanywa watumwa wa ngono. Ripoti ya UNICEF imeashiria jinsi watoto wanavyotumiwa na makundi ya wanamgambo kama askari vitani huko barani Afrika.
Ripoti hiyo imeashiria mapigano ya Sudan Kusini na kubainisha kwamba, takribani watoto elfu kumi na mbili wametumiwa kama askari vitani. Umoja wa Mataifa umesisitiza juu ya ulazima wa kuweko juhudi za kusimamia zoezi la kuwaokoa watoto hao toka katika mikono ya makundi ya wanamgambo. Sehemu nyingine ya ripoti hiyo imeashiria jinsi makundi ya kigaidi huko Syria na Iraq yanavyowatumia watoto wadogo katika mashambulio yao. Ripoti hiyo inatolewa katika hali ambayo, hivi karibuni taasisi ya kujitegemea ya kuwatetea watoto "Save the Children" yenye makao yake huko Dakar, mji mkuu wa Senegal, ilitangaza kuwa takriban watoto elfu sita hadi 10 wanatumikishwa jeshini huko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kwa kuzingatia kuwa hii leo silaha na zana za kivita zimekuwa zikipatikana kwa urahisi mno, suala la kuwatumikisha watoto limekuwa suala jepesi sana, hasa kwa kutilia maanani kwamba, watoto hao wanaweza pia kutumika katika kubeba silaha hizo.
Ni kwa kuzingatia hali hiyo ndio maana hivi sasa kumeajitokeza harakati nyingi za kuwatetea watoto katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. Taasisi mbalimbali zimeanzisha kampeni tofauti kwa lengo la kusitisha kutumikishwa watoto jeshini ili kuwaokoa watoto hao ambao ni taifa la kesho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Kutumiwa watoto vitani katika nchi zaidi ya 20 duniani. Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top