MAKAMANDA WA MIKOA MITATU YA MWANZA, SIMIYU NA SHINYANGA WAVUNJA NGOME HATARI YA MTANDAO WA UJAMBAZI
POLISI wa
mikoa ya Mwanza, Simiyu na Shinyanga wamefanikiwa kusambatarisha mtandao
wa ujambazi kwenye mikoa hiyo baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa wa
ujambazi sugu, Njile Samweli (46) mkazi wa kijiji cha Lyoma, Bariadi
mkoani Simiyu aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu.
Sambamba na kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo wa ujambazi, pia watuhumiwa
watano wanashikiliwa, bunduki moja yenye namba PB 3402 aina ya SMG na
risasi 331 na kwamba operesheni ya kina inaendelea kwa lengo la
kuwakamata watuhumiwa wote pamoja na silaha wanazotumia.
Wakizungumza kwa pamoja Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Valentino
Mlowola alisema Januari 5, mwaka huu majira ya saa 7 mchana walimkamata
Mabula Lyagwa (36) akiwa na jeraha la risasi kwenye bega lake la kulia
baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema.
Alisema mtiliwa shaka huyo alipohojiwa alisema kuwa jeraha hilo alipigwa
risasi na jambazi mwenzake aitwaye Njile Samweli wakati wakifanya tukio
la ujambazi katika kijiji cha Idukilo kata ya Mwadui Luhumbo wilayani
Kishapu mkoani Shinyanga Januari 5, saa sita za usiku.
Alisema kutokana na maelezo hayo kikosi cha upelelezi mkoani hapa
kiliungana na mikoa mingine na kufanya msako uliofanikiwa kumkamata
Njile Samweli ambapo alipohojiwa alikiri kuhusika na matukio mbalimbali
ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika mikoa ya Simiyu, Mwanza,
Shinyanga, Tabora na Singida.
Alisema mkoani hapa, mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake wamefanya matukio
mbalimbali ya uhalifu ambapo Agosti mwaka jana walivamia nyumba ya
kulala wageni kwenye kisiwa cha Bulubi, wilayani Ukerewe na kupora Sh
milioni 3.5 za wafanyabiashara wa dagaa.
0 maoni:
Chapisha Maoni