Hatua ya kwanza ya ndoto ya kuzama
katika elimu ya mabinti pacha walioungana kiwiliwili, Consolata na Maria
Mwakikuti (18) wa Kijiji cha Ikonda wilayani Makete mkoa mpya wa Njombe, inatarajiwa kutimia
Novemba mwaka huu, wakati mabinti hao watakapofanya mtihani wa kuhitimu kidato
cha nne.
Itakumbukwa kwamba walipokuwa
wakimaliza elimu ya msingi mwaka 2009 kijijini kwao Ikonda, walikuwa na umri wa
miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja walisema wanataka kuwa wasomi
waliobobea katika utaalamu wa kompyuta. Lakini, kwa sasa, wanasema wanatamani
kufanya kazi ya Ukatibu Muhtasi.
Wanafunzi hao ambao mwaka 2010
walichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Dar es
Salaam.
Kwa sasa wanasoma katika Shule ya
Sekondari ya Maria Consolata iliyopo Kidabaga wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Shule hiyo inamilikiwa na Kituo cha
Nyota ya Asubuhi ya Wamisionari Wakatoliki wa Italia, kinachosaidia kuwatunza
watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari
hii shuleni hapo hivi karibuni, walisema wanafurahi kuwa miongoni mwa
watahiniwa watakaofanya mtihani huo wa kidato cha nne mwaka huu.
"Tunafurahi, tunajiandaa
tunasoma kwa bidii, mtihani uko karibu tunataka tufaulu vizuri masomo yetu, ili
ile ndoto yetu ya kuwa Makatibu Muhtasi itimie," walisema Maria na
Consolata, ambao wanatumia baiskeli maalumu kuwapeleka darasani, ambako pia
wana kiti maalumu.
Pacha hao wameshangaza watu wengi
kwa jinsi walivyo, ambapo kila mmoja ana madaftari yake. Wakati wa kufanya
mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na
mwingine huandika.
"Wala hatupati shida tumezoea,
kila mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria
anaandika kwa mkono wa kulia," anasema Consolata, ambaye anaonekana kuwa
mchangamfu zaidi.
Shule hiyo ina wanafunzi wa kidato
cha kwanza hadi cha nne. Ilianzishwa mwaka 2006 na hivi sasa ina jumla ya
wanafunzi 183. Wote wanaishi kituoni hapo na wote wanatoka kwenye mazingira
magumu.
Changamoto kubwa iliyokuwa shuleni
hapo ni ukosefu wa nishati ya umeme, ambapo uongozi wa shule na kituo hicho
unalazimika kutumia jenereta na umemejua, jambo ambalo mapema wiki hii Wakala
wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA), imewaondolea adha kwa kuwapelekea umeme.
Pacha hao walizaliwa mwaka 1996
wakiwa wameungana katika Hospitali ya Ikonda wilayani Makete mkoani Iringa.
Walifaulu mtihani wa darasa la saba
mwaka 2010, ambapo kila mmoja alipata alama 151, ingawa walitofautiana
ufaulu kwenye masomo yao.
Katika somo la Maarifa ya Jamii,
Consolata alipata alama 29 na Maria alama 25, kwenye somo la Kiingereza, Maria
alipata alama 36 na kumzidi Consolata aliyepata alama 34, wakati kwenye somo la
Sayansi, Maria alimzidi Consolata kwa kupata alama 31 dhidi ya 29.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
iliwapanga pacha hao kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari
Jangwani jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo hawakujiunga na sekondari
hiyo, kutokana na hali yao na pia umbali kutoka Iringa hadi Dar es Salaam.
Ndipo Wamisionari hao wakawachukua mwaka 2011 na kuanza kidato cha kwanza.
Walizaliwa kwenye Hospitali ya
Misheni ya Ikonda mwaka 1996. Lakini, taarifa zao hazikufahamika hadi pale
walipoandikishwa kuanza elimu ya msingi Ikonda na kutafutiwa mlezi wa
kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa bado wadogo.
0 maoni:
Chapisha Maoni