Jumamosi, 20 Septemba 2014

Mtoto apigwa radi mchana kweupe na kufariki Dunia,wengine wajeruhiwa

Mtoto apigwa radi mchana kweupe na kufariki Dunia,wengine wajeruhiwa

 Majeruhi Bi.Noelia Bulembo, mwanae Japhet Seth na Riziki Daudi, Mwanafunzi wa Darasa la Tano katika Shule ya Msingi Tambuka Reli, wakiwa katika wodi namba 8 ya Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni, baada ya kupigwa na radi

MTOTO mwenye umri wa miaka mitatu amefariki Dunia na Watu wengine watatu kujeruhiwa katika matukio mawili tofauti ya kupigwa radi huko katika Kijiji na Kata ya Kazuramimba Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.

Tukio hilo lilitokea jana Septemba 19, majira ya saa kumi jioni, ambapo kwa nyakati tofauti radi ilipiga nyumbani kwa Bw.Seth Kiyoya mkazi wa Kitongoji cha Kilelema C, na wakati huo huo kupiga nyumbani kwa Bw.Jiresi, mkazi wa Kitongoji cha Tambuka Reli kijijini hapo.

Katika tukio la kwanza katika Kitongoji cha Kilelema C, Bi.Noelia Bulembo, mwenye umri wa miaka 30 na Watoto wake wawili, Japhet Seth miaka 5 na Rajabu Omary miaka 3,walipigwa na radi ambapo Rajabu Omary alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika Zahanati ya Kijiji cha Kazuramimba.

Aidha katika tukio la pili Mwanafunzi wa Darasa la Tano katika Shule ya Msingi Tambuka Reli katika Kitongoji cha Tambuka Reli, Riziki Daudi mwenye umri wa miaka 14, alijeruhiwa kwa kupigwa radi wakati akicheza na wenzake nyumbani kwa Bw.Jiresi.

Akieleza tukio hilo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni, walipolazwa kwa ajili ya matibabu Bi.Noelia Bulembo alisema: “Ilikuwa jana saa kumi jioni mimi nikiwa nimetoka kuoga, tulisikia muungurumo ndipo radi ilipopiga ikatoboa ukuta na kuingia ndani wakati nimesimama ikawa imenipitia kwenye miguu nikasikia miguu inawaka moto. Kulikuwa hakuna mawingu wala mvua haikunyesha, jua lilikuwa linawaka.”

Aliongeza kuwa wakati huo watoto wake wawili walikuwa nje ambapo walipigwa na kujeruhiwa na radi kisha kukimbizwa katika Zahanati ya Kijiji cha Kazuramimba kwa matibabu, lakini mmoja alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa kwenye zahanati hiyo.

Muuguzi Msaidizi katika Wodi namba nane ya Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni, Bi.Venenciana Gervas Mtaki, alithibitisha kupokea majeruhi hao wa radi, ambao alisema hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma, ACP Jaffari Mohamed, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Mtoto apigwa radi mchana kweupe na kufariki Dunia,wengine wajeruhiwa Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top