MCHAKATO WA BUNGE LA KATIBA NI HALALI .
MCHAKATO WA BUNGE LA KATIBA NI HALALI – WAZIRI MKUU
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema mchakato wa Bunge la Katiba unaoendelea hivi
sasa ni halali na kwamba mchakato huo ni wa kisheria.Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Septemba 21, 2014) wakati akizungumza
na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya
uzinduzi wa dayosisi mpya ya Ziwa Tanganyika ya Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuwekwa wakfu Askofu Ambele Anyigulile
Mwaipopo aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo. Dayosisi hiyo inakuwa ya
24 kwa kanisa hilo. Waziri
Mkuu alikuwa akitoa ufafanuzi wa hoja ya Askofu Mwaipopo aliyetaka
maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe na Bunge Maalum la
Katiba lisitishwe kama ambavyo Jukwaa la Katiba limetaka na tamko la
Jumuiya za Kikristo Tanzania (CCT) limetamka.
Waziri
Mkuu alisema: “Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume hiyo siyo
Katiba bali mawazo yaliyokusanywa ambayo yanapaswa kupitiwa na chombo
kingine cha kisheria ambacho ni Bunge Maalum la Katiba. Mchakato huu
halali na mchakato huo ni wa kisheria.”
Alisema
muda ambao Tume hiyo ilipewa haukuwa mrefu sana kwa hiyo isingekuwa
rahisi kwao kuzingatia kila eneo linalogusa maisha ya Watanzania. “Mfano
suala la ardhi halikuelezwa vizuri katika rasimu lakini kwa sasa
limeelezwa vizuri jinsi ardhi inavyoweza kumnufaisha Mtanzania kwenye
kilimo, ufugaji, uvuvi na rasilmali misitu,” alisema.
Alisema
kinachowachanganya Watanzania ni suala la Serikali mbili au tatu lakini
katika makabrasha ya Tume ambayo wajumbe wote walipewa, suala la
Muungano halikupewa kipaumbele na Watanzania wengi waliotoa maoni yao.
“Kulikuwa na masuala makubwa sita. Suala la ukiukwaji wa haki za
binadamu ndilo lilikuwa namba moja, suala lililopewa umuhimu wa pili
lilikuwa ni la matatizo ya huduma za jamii na hilo la muungano
lilichangiwa na kundi dogo sana,” alisema.
Alisema
kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Jaji Warioba watu waliotaka Muungano
wa Serikali tatu ni kati ya asilimia 12 na 13. “Haiwezekani kwa takwimu
zile za asilimia 12 hadi 13 za kutaka Serikali tatu, iamuliwe jumla
kwamba ni kwa niaba ya Watanzania wengi.”Ili kukidhi shauku ya wengi,
Waziri Mkuu alisema yuko radhi ifanyike kura mahsusi ya kuwaomba
Watanzania waseme kama wanataka Muungano na tena uwe ni wa aina gani.
“Baba
Askofu amesema tusitishe Bunge la Katiba, hivi sababu hasa ya kusitisha
ni nini? Je sote tunajua hoja iliyowafanya wenzetu watoke nje na
kususia ni ipi? Katika muda wa kuchangia kulikuwa na dakika 40 za wengi,
dakika 20 za wachache na wakapewa dakika nyingine 30 za kuchangia. Muda
ule ni mwingi mno kama hujaweka mchango wako kwenye maandishi. Badala
yake, sote tulishuhudia kukashifiana, kejeli na kukashifiana.”
Aliwasihi
Maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wa dini waliohudhuria uzinduzi
huo waendelee kuumboe mchakato huo ili uishe vizuri.
Katika
hotuba yake, Waziri Mkuu alimuomba Askofu huyo mpya apokee jukumu hilo
kwa mikono miwili na kumuahidi kuwa Serikali itasaidiana naye kuwaongoza
Watanzania walioko kwenye dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha
mikoa ya Rukwa na Katavi eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba
75,140. Kati ya hizo km. za mraba 27,713 ni za mkoa wa Rukwa na km. za
mraba 47,527 ni za mkoa wa Katavi.
Alisema
katika dayosisi hiyo mpya kuna changamoto nyingi kama vile za malezi ya
vijana na watoto, tabia ya watu kutopenda kufanya kazi hasa vijana,
kukosekana kwa injili kwenye maeneo wanayoishi wafugaji na suala la
imani za ushirikina.“Asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana na wao ndiyo
Taifa la leo. Ukiangalia mavazi ya vijana wa kike (vimini) na wa kiume
(mlegezo) hutamani kuwaangalia mara ya pili. Msingi mkubwa wa
kuwabadilisha hawa wote ni malezi ya kiroho. Una changamoto pia ya
kufikisha neno la Mungu kwa wafugaji ambao ni wengi eneo hili lakini
hawana muda wa kuabudu na wengi wao hawalijui neno la Mungu, wako bize
na mifugo yao.”“Lakini changamoto kubwa kuliko zote ni ya kubadili
mtazamo wa jamii kuhusu Mkoa wa Rukwa hasa kwenye suala la ushirikina.
Mtu hata kama hatoki huku bado ataweka bango akisema Mganga machachari
kutoka Sumbawanga. Baba Askofu naomba tushirikiane kupiga sana vita
imani hizi potofu kwa sababu zinachangia mauaji ya wazee na walemavu wa
ngozi,” alisisitiza Waziri Mkuu.Mapema, akitoa hotuba yake ya kwanza
mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwaipopo aliiomba Serikali
isifumbie macho viashiria vyote vya upotevu wa amani kwani amani ni
tunda la upendo na wala haipatikani kwa ncha ya upanga.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
DAR ES SALAAM.
JUMAPILI, SEPTEMBA 21, 2014.
0 maoni:
Chapisha Maoni