Kocha mpya Stars amchenjia Yondani
KOCHA mpya wa Taifa Stars, Mart Nooij, ameanza kazi na beki
mahiri wa Tanzania, Kelvin Yondani. Beki huyo awali aliitwa kwenye
kikosi kilichopigwa mabao 3-0 na Burundi, lakini akaingia mitini.
Mart alivyokabidhiwa timu na majina akalikuta jina
la Yondani bado lipo akawaangalia viongozi wa ufundi wa Shirikisho la
Soka la Tanzania (TFF) akalipiga mstari kwa nguvu jina la Yondani baada
ya kuonyesha kukerwa na kitendo hicho akisema wazi kuwa ni utovu wa
nidhamu.
Kocha huyo ameongeza wachezaji tisa katika kikosi
hicho kinachojiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi itakayochezwa
Mei 4 mwaka huu katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Wachezaji walioongezwa ni Edward Charles Manyama
(JKT Ruvu), Elias Maguli (Ruvu Shooting), Hassan Dilunga (Yanga),
Hussein Javu (Yanga), John Bocco (Azam), Kelvin Friday (Azam), Oscar
Joshua (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (AC Cannes,
Ufaransa).
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Pemium
Lager, inaingia kambini leo Jumatatu jijini Mbeya kujiandaa kwa mechi
dhidi ya Malawi.
Wakati huohuo, Tanzania imepangiwa kucheza na
Zimbabwe katika raundi ya pili ya mechi za mchujo kuwania tiketi ya
kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika
Morocco mwakani.
Stars itaanzia nyumbani ambapo mechi ya kwanza
itachezwa kati ya Mei 16 na 18 wakati ile ya marudiano itachezwa Harare
kati ya Mei 30 na Juni Mosi.
Katika hatua nyingine, Stars juzi Jumamosi ilitoa kali baada ya kupiga mashuti matatu tu katika mechi nzima dhidi ya Burundi.
Katika mchezo huo wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam, Stars ikiiwa chini ya kocha Salum Mayanga
ilimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikipiga shuti moja pekee
lililoshindwa kulenga lango. Kiungo mshambuliaji, Simon Msuva, ndiye
aliyelipiga.
Katika kipindi hicho Burundi ilipiga mashuti manne
ambapo mawili yalilenga lango na mojawapo likazalisha bao lililofungwa
na Didier Kavumbagu.
Kipindi cha pili licha ya Stars kufanya mabadiliko
kadhaa hali ilizidi kuwa mbaya ambapo ilipiga mashuti mawili pekee yote
yakishindwa kulenga lango, moja lilipigwa na Haroun Chanongo na jingine
lilipigwa na Ramadhan Singano 'Messi' ambalo lilitoka nje. Burundi
ilikipiga matatu mawili na mawili yakazaa mabao yaliyofungwa na
mshambuliaji Amissi Tambwe na kiungo mkabaji Ndikumana Yusuf.
Akizungumzia hali hiyo, Mayanga alisema: "Tunataka
kuwajaribu baadhi ya wachezaji wetu ambao huu ndiyo ulikuwa mchezo wao
wa kwanza wa kimataifa, tumeona kila kitu sasa tunaenda kuyafanyia kazi
mapungufu yaliyojitokeza."
0 maoni:
Chapisha Maoni