MAMBO
YA KUTAFAKARI KATIKA KIPINDI HIKI CHA CHRISTMAS
Heri ya Christmas mpenzi msomaji!
Mathayo 1:21 ‘Naye atazaa mwana,
nawe utamwita jina Yesu, maana, yeye ndiye atayewaokoa watu wake na dhambi zao’.
Hakika hii ni sherehe ya ajabu na ya
kipekee sana maishani kwetu. Kila mwaka ifikapo Desemba 25, Wakristo duniani
kote huadhimisha sherehe ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Naam kuna
mambo mengi ambayo hufanyika katika siku hii au katika kipindi cha maadhimisho
ya siku kuu hii. Wapo wanaojua maana ya siku hii na wapo ambao wameigeuza siku
hii kuwa chukizo mbele za Mungu kutokana na matendo yao.
Hivyo tunapoadhimisha sherehe hii
katika mwaka huu, yafuatayo ni mambo ambayo tumeona ni vema tukakumbushana nayo
ni;
- Mwokozi amezaliwa
Mstari wa 21 wa kitabu cha Mathayo
unatueleza kusudi la kuja kwake Bwana wetu kuwa ni kuwaokoa watu wake na dhambi
zao. Naam ni upendo wa pekee sana kwa Bwana Yesu kuacha heshima na utukufu
mbinguni na aje azaliwe, afe na kufufuka ili tupate waokovu. Kwa sababu hiyo
kama bado hujaokoka ni vema ukafanya maamuzi ya kuokoka. Haukuwa uamuzi rahisi
kwa Yesu kuacha heshima na enzi mbinguni aje kwa ajili yetu. Na wewe uliyeokoka
usiendelee kuishi maisha ya dhambi kama asiyemjua Mungu.
- Boresha uhusiano wako na Roho Mtakatifu
Biblia inasema ‘Kuzaliwa kwake
Yesu kulikuwa hivi, Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla
hawajakaribiana, alionekana na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu’ (Matahyo
1:17)
Mimba ya Bwana wetu ndani ya Mariamu
ilikuwa ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Nasi tunajua ya kwamba, Roho Mtakatifu
ni Mungu, na kwa sasa yeye ndiye ambaye yupo duniani analiandaa kanisa la Bwana
na kuhakikisha kusudi la Mungu kupitia ‘mtu’ linafanikiwa. Naam ni muhimu sana
kila aliye wa Kristo kuhakikisha kwamba mahusiano yake na Roho Mtakatifu
yanakuwa mazuri daima. Naam tumia kipindi hiki kumshukuru Mungu kwa siku hii na
kujenga msingi mzuri wa mahusiano na Roho Mtakatifu kuanzia sasa na kuendelea.
- ‘Christmas’ siyo siku ya kufanya uovu
Ni vema watu wote wakatambua kwamba
siku hii siyo siku ya kufanya kila namna ya uchafu na dhambi ambazo wanadamu
wamezoea kufanya katika siku hii. Ni vema siku hii ikaheshimika sana, maana
ndiyo siku ambayo dunia ilipokea mwokozi wa ulimwengu. Naam siku ambayo
ufumbuzi wa dhambi ulikuja kwa wanadamu duniani. Shetani amekuwa akijaribu
kuharibu sifa/ picha (image) ya siku hii, kwa kuwafanya wanadamu wapange
kufanya kila namna ya machikizo mbele za Mungu wetu. Ole kwao wafanyao hayo,
naam tulio wa Kristo Yesu tunajua maana ya siku hii na tunaona fahari kwa ajili
ya siku hii, utukuzwe Baba kumtoa mwanao, utukuzwe mwana kwa kukubali kuja ili
tupate kuwa warithi wa ufalme wako tungali dunani na kisha uzima wa milele.
- Fanya tathmini ya wokovu wako
Kwa kawaida wanadamu hufanya
tathimini ya mambo mbalimbali katika maisha yao. Ni wachache sana ambao hufanya
tathmini juu ya maisha yao ya wokovu ndani ya Kristo. Katika mwaka 2013, je
umekuwa Balozi wa kweli wa Kristo katika nyumba, ofisi, mji au Taifa lako na
kwa wale wanaokuzunguka kila siku? vipi kuhusu uaminifu, je umekuwa muaminifu
kwa kiasi gani mbele za Mungu, je unaweza kusema umeishi maisha ya ushuhuda
katika Kristo Yesu nk.
Vipi kuhusu mahusiano yako na
wenzako, je kuna amani, vipi kuhusu zaka na dhabihu? Kwa kifupi katika vigezo
vyote vya wokovu alama zako zikoje, ingekuwa unajiwekea alama katika mia moja
ungejiwekea ngapi? na Bwana naye angekuwekea ngapi? Naam pale unapoona
hukufanya vema, omba toba na kuomba nguvu mpya ya kukusaidia kipindi
kinachofuata.
MIMI NA FAMILIA YANGU TUNAWATAKIA KHERI YA CHRISTMASS NA MWAKA MPYA.


0 maoni:
Chapisha Maoni