Jumamosi, 19 Oktoba 2013

Mbio za mitumbwi za Balimi kukata utepe Kigoma J’mosi





MASHINDANO ya mbio za mitumbwi ya Balimi Extra Lager 2013 yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi keshokutwa katika ufukwe wa Kibirizi mjini Kigoma.
Mashindano hayo ya kupiga makasia, yanafanyika kwa mwaka wa 14 chini ya udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia Balimi Extra Lager, yamekuwa na hamasa na msisimko mkubwa kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah, alisema lengo hasa la Bia ya Balimi Extra kudhamini mashindano hayo ni kufurahi pamoja na wakazi wa Kanda ya Ziwa hususan wale ambao ni wavuvi.
“Mashindano haya yanaenzi na kulinda tamaduni zetu zisipotee, yanajumuisha watu mbalimbali kukutana, kufahamiana na kufurahi kwa pamoja na hii inasaidia sana kuimarisha amani na upendo baina yetu. Amani ni nguzo muhimu sana kwa taifa letu,” alisema huku akisisitiza umuhimu wa michezo katika kujenga afya bora.
Alifafanua kwamba, mwaka huu mashindano hayo yatahusisha miji mitano na yataanza rasmi mchakato wake Jumamosi hii Kigoma, kisha kuelekea Bukoba Novemba 2, Mwanza Novemba 9, Ukerewe Novemba 16, Musoma Novemba 23 kisha mashindano ya Kanda Desemba 7 jijini Mwanza ufukwe wa Mwaloni.
Alizitaja zawadi kwa washindi ngazi ya mkoa upande wa wanaume kuwa ni sh 900,000 kwa wa kwanza, wa pili sh 700,000, wa tatu sh 500,000, huku wa nne akipata sh 400,000 wakati wa tano hadi 10 watajipoza kwa sh 250,000 kila mmoja.
Kwa wanawake bingwa atapata sh 700,000, wa pili sh 600,000, wa tatu sh 400,000 na wa nne sh 300,000 wakati wa tano hadi 10 watapata sh 200,000 kila mmoja.
Ngazi ya Kanda, bingwa atapata sh 2,700,000 wa pili sh 2,300,000, wa tatu sh 1,700,000 wa nne sh 900,000 huku wa tano hadi 10 watapata sh 400,000 kila mmoja kwa upande wa wanaume.
Kwa wanawake, bingwa atapata sh 2,300,000 wa pili sh 1,700,000, wa tatu sh 900,000, wa nne sh 700,000, huku wa tano hadi 10 watajipoza kwa sh 250,000 kila mmoja.
Naye Mratibu wa mashindano hayo, Peter Zakaria, alisema maandalizi yako vema na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi hiyo Jumamosi.



  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Mbio za mitumbwi za Balimi kukata utepe Kigoma J’mosi Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top