COASTAL Union itamkosa beki wake tegemeo wa pembeni Miraj Adam (pichani kulia) katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho dhidi ya Majimaji kesho.
Coastal watakuwa wageni wa Majimaji kesho Uwanja wa Majimaji Songea na beki wake Miraj anayecheza kwa mkopo kutoka Simba hakusafir4i na timu kwa sababu ya matatizo ya kifamilia.
Miraj amefiwa na bibi yake mzaa mama na tayari yuko Morogoro kwa shughuli za mazishi. “Siwezi kabisa kuwahi hiyo mechi, ila nawatakia kila la heri wenzangu,”amesema.
Kwa ujumla Ligi Kuu ya Bara inatarajiwa kuendelea kesho mechi mbili, ikiwemo Azam FC kumenyana na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ni ya kiporo na Azam FC imeamua kucheza baada ya maombi yao ya awali kuomba mchezo huo usogezwe mbele kwa ajili ya kupata muda wa kujiandaa kuikabili Esperance kukataliwa.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema jana kwamba baada ya kulazimishwa sare na Toto Africans, leo kikosi hicho kitashuka uwanjani kikijipanga kusaka ushindi na kuendelea kuwa kwenye mbio za kutwaa ubingwa.
Hall amesema kwamba endapo watapoteza pointi kwenye mechi ya leo, safari ya kuivua Yanga ubingwa itakuwa ni ngumu kwa sababu wanazidiwa mabao na mabingwa hao watetezi.
"Hakuna mechi rahisi, tutashuka uwanjani kesho (leo) kwa ajili ya kusaka ushindi, mazingira ya mechi iliyopita jijini Mwanza hayakuwa mazuri, tumerudi kwenye Uwanja wetu ambao tumeuzoea, hatutarudia makosa," alisema kocha huyo ambaye ni raia wa Uingereza.
Naye kocha wa Ndanda FC, Meja mstaafu, Abdul Mingange, alisema kwamba mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao wako kwenye mbio za ubingwa huku wao wakijiepusha na janga la kushuka daraja.
"Wasitarajie mteremko, tukicheza mpira wa haki, naamini hatutakosa pointi kwenye mechi ya kesho (leo)," Mingange alisema.
Simba iliyocheza mechi 24 bado inashikiliwa usukani wa ligi baada ya kuwa na pointi 57 na kufuatiwa na Yanga yenye pointi 53 huku Azam ikishika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 51.
0 maoni:
Chapisha Maoni