Na Baraka Mbolembole
Wakati ‘vigogo wa ligi’ Yanga SC, Simba SC na Azam FC wakitaraji kushuka uwanjani wikendi hii kuendeleza vita yao ya kuwania ubingwa, timu nyingine 13 pia zitakuwa viwanjani kuwania pointi 3 muhimu.
Vita kali nyingine msimu huu inataraji kuwepo katika eneo la kushuka daraja. JKT Ruvu, African Sports, na Coastal Union zinaweza kushuka endapo hazitafanya jihada kujinasua katika nafasi walizopo sasa (nafasi ya 16 kwa JKT Ruvu, nafasi ya 15 kwa Sports na nafasi ya 16 kwa Coastal kabla ya mechi za wikendi hii)
KAGERA SUGAR v JKT MGAMBO
Kocha, Bakari Shime ametishia kuachia nafasi yake katika timu ya Mgambo kwa madai ya kuingiliwa katika majukumu yake ya kazi. Mgambo imekosa matokeo katika michezo kadhaa sasa na wakiwa katika nafasi ya 12 na pointi zao 18 watakuwa wageni wa Kagera Sugar katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga siku ya Jumamosi hii.
Kagera chini ya kocha mzoefu, Adolf Richard imeonekana kuzinduka katika mzunguko wa pili na kushinda baadhi ya michezo yake kiasi cha kuwaondoa mwisho wa msimamo hadi katika nafasi ya 13 wakiwa na alama 17 (pointi moja nyuma ya Mgambo) Katika mazingira ya ligi jinsi yalivyo na huku zikiwa zimesalia mechi kumi kabla ya kumalizika kwa msimu timu hizo mbili (Kagera na Mgambo) zote zipo katika eneo baya.
Kila timu inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuongeza pointi muhimu. Kagera na Mgambo zimeshinda gemu nne tu kati ya 20 walizokwisha cheza. Mgambo imefanikiwa kutoa sare katika michezo 6 wakati Kagera imekutana na matokeo hayo katika gemu 5.
Timu zote zimekuwa zikiruhusu magoli mengi, Kagera imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara 23 wakati Mgambo wameokota mpira nyavuni kwao mara 25. Mgambo wamekuwa wakibebwa na safu yao ya mashambulizi ambayo imefanikiwa kufunga magoli 16.
Kagera ni timu iliyofunga magoli machache katika ligi msimu huu nyuma ya African Sports. Kikosi hicho cha Adolf kimefanikiwa kufunga magoli 11 tu kabla ya mechi yao ya Jumamosi hii. Ukitazama namna tofauti ya pointi ilivyo kati ya timu hizo na zile 3 za mwisho ni wazi timu itakayopoteza mchezo huo itakuwa imejishusha chini zaidi.
JKT Ruvu ndiyo wanaburuza mkia wa ligi ikiwa na pointi 15, inafuatia Sports na ndugu zao wa Tanga, Coastal Union zenye pointi 16 kila timu. Kagera v Mgambo ni vita ya kuepuka kushuka daraja tu si vinginevyo.
JKT RUVU v MWADUI FC
Ukiachana na ujio wa timu mpya kama Mbeya City FC, Stand United, Ndanda SC, Ni timu tano tu ambazo hazijawahi kushuka daraja tangu zilipopanda ligi kuu Tanzania Bara. Yanga SC, Simba SC, Mtibwa Sugar, Azam FC hazijawahi kushuka daraja lakini itakuwa bahati sana kama JKU Ruvu itakwepa ‘mkasi’ msimu huu na kunusurika kushuka.
Kikosi cha kocha Abdallah ‘King’ Kibadeni kimefanikiwa kushinda michezo mitatu tu kati ya 20 waliyokwisha cheza na kipo nafasi ya mwisho kabisa ya msimamo kikiwa na alama 15 tu. Kitawakaribisha Mwadui FC iliyo nafasi ya nne katika uwanja wa Karume, Dar es Salaam na kama watashindwa kupata ushindi watakuwa hatarini zaidi.
Mwadui chini ya Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ inahitaji kumaliza katika nafasi 3 za juu msimu huu, wameshinda gemu 9, wamepoteza mara sita na kulazimishwa sare 5, wamekusanya pointi 32 (pointi 13 nyuma ya Simba iliyo nafasi ya 3) Si rahisi kwa kikosi cha Julio kuwania ubingwa msimu huu lakini wanakwenda Dar es Salaam kuhakikisha wanakusanya pointi 3 muhimu.
JKT Ruvu wamejitahidi kufunga magoli lakini ndiyo timu iliyoruhusu magoli mengi zaidi hadi sasa. Imefunga magoli 19 (mawili pungufu ya Mwadui FC) lakini imeruhusu nyavu zake mara 35 hilo ndilo linaloendelea kuwaangusha.
Wanapaswa kuongeza umakini katika ngome yao kama wanataka kuendelea kubaki VPL msimu ujao. JKT Ruvu v Mwadui FC hii ni vita ya kushuka daraja kwa JKT Ruvu, ngazi ya kwenda top3 kwa Mwadui FC.
AFRICAN SPORTS v MAJIMAJI FC
Kuna mechi nyingi kali wikendi hii na gemu hii itakayopigwa katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga itakuwa kali, kali kupita maelezo. Timu zote mbili (Sports na Majimaji) zilipanda VPL msimu huu baada ya kufanya vizuri katika ligi daraja la kwanza msimu uliopita, lakini mambo si mazuri sana upande wao hadi sasa na zitakutana kila timu ikiwa katika malengo ya kushinda ili kukimbia ‘kushuka.’
Sports ndiyo timu iliyofunga magoli machache zaidi katika VPL hadi sasa, ikiwa nafasi ya 15 na pointi zao 16 timu hiyo ya Tanga imefanikiwa kufunga magoli 7 tu katika michezo 20. Wameshinda mara 4, sare 4 na kupoteza michezo 12.
Majimaji chini ya kocha Kally Ongalla ipo nafasi ya 11 lakini kuna tofauti ya pointi 3 tu kati yao na Sports hivyo wanaweza kuporomoka hadi nafasi ya 15 ikiwa watapoteza mchezo huo.
Timu hiyo ya Songea, Ruvuma imekuwa dhaifu mno katika kuzuia kwani hadi sasa wameruhusu magoli 32 na wamefunga 12 tu katika michezo 20. Hii ni vita hasa ya kuepuka kushuka daraja na inataraji kuwa ngumu na kali sana.
TOTO AFRICANS v NDANDA SC
Toto walianza vizuri lakini wanasotea ushindi wa kwanza baada ya kucheza zaidi ya mechi 9 bila kushinda. Ikiwa nafasi ya 9 na pointi 22, timu hiyo itawakaribisha Ndanda SC katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika mechi nyingine ya kukimbia ‘eneo la hatari.’
Ndanda ipo nafasi ya 8 na pointi 23 bado haiwezi kujiona iko salama kwa kuwa ni tofauti ya pointi 8 tu iliyopo kati yao na JKT Ruvu iliyo nafasi ya mwisho. Ushindi utawafanya wafikishe alama 27 hivyo wanaweza kuwa salama endapo watashinda mchezo huo.
MTIBWA SUGAR v COASTAL UNION
Wiki iliyopita timu hizo mbili zilikutana katika hatua ya 16 bora ya michuano ya FA na Coastal ilifanikiwa kupata ushindi wa 1-0 katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Kocha, Ally Jangalu wa Coastal alisema kwamba angefurahi zaidi kama ushindi huo ungekuwa katika ligi kuu kwani ungewaongezea pointi 3 muhimu na kuwaondoa katika nafasi mbaya waliyopo.
Coastal imepopeza mechi kumi, imeshinda mara 3 tu na hivyo wamejikuta wakibaki katika nafasi ya 14 na alama zao 16 sawa na Sports iliyo nafasi ya 15. Ushindi utawafanya kufufua hali yao na kurudisha matumaini ya kuendelea kubaki katika VPL msimu ujao.
Mtibwa chini ya Mecky Mexime kwa mara nyingine wameshindwa kuwa washindani wa ubingwa licha ya kuanza msimu kwa kasi. Ikiwa imeporomoka hadi nafasi ya 6 na pointi zao 30, bila shaka watataka kulipa kisasi kwa Coastal na kurudisha matumaini ya kumaliza top 3 msimu huu.
0 maoni:
Chapisha Maoni