Jumapili, 20 Machi 2016

Utata watanda kutoweka kwa mwandishi, wadau walaani

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa
Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Onesmo Olengurumwa akitoa tamko la kulaani kutekwa na kupelekwa kusikojulikana mwandishi, Salma Said wakati wa mkutano na wanahabari Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga. Picha na Salim Shao 
Dar es Salaam. Utata umezingira suala la kutoweka kwa mwandishi wa habari, Salma Said ambaye juzi ilisemekana alichukuliwa na watu wasiojulikana kwenye Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume na hadi sasa hajulikani alipo, ingawa amekuwa akiongea kwa simu na mumewe.
Si mumewe, Jeshi la Polisi au wafanyakazi wenzake wanaojua sehemu ambayo mwandishi huyo wa Mwananchi yupo hadi sasa, lakini mumewe anasema watu waliomteka humruhusu aongee naye anapotaka kufanya hivyo, lakini hapatikani anapotafutwa na wengine.
Mwandishi huyo alimpigia simu mumewe juzi saa 6.00 mchana akiwa ofisini mjini Unguja na kumweleza kuwa hajisikii vizuri kwa sababu ana matatizo ya moyo. Mumewe akamshauri aende Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Mume wake huyo, Ali Salim Khamis, alimpitia ofisini saa 7,30 mchana kumpeleka uwanja wa ndege tayari kwa safari ya Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya Kampuni ya Auric Air, ambayo ilitakiwa iondoke 08.05 mchana.
Hata hivyo, ilichelewa na iliondoka Zanzibar saa 08.45. Haijulikani sababu za ndege hiyo kuchelewa kuondoka kwa takriban dakika 40. Kwa mujibu wa mume huyo, saa 9:00, Salma alimuandikia ujumbe uliosema kuwa amekamatwa akiwa uwanja wa ndege, lakini hakufafanua ni Zanzibar au Dar es Salaam. Kwa mujibu wa mume huyo, Salma aliwahi kumwambia mumewe kuwa anapata vitisho mara kwa mara kutokana na anayoyaandika kwenye mitandao, hali iliyofanya Khamis aende kuripoti kituo cha Polisi cha Madema.
Khamis alisema jana kuwa aliwasiliana na mkewe saa tisa alfajiri ya kuamkia jana na baadaye saa nne asubuhi akimwambia yuko salama.
Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema jana kuwa alikuwa na taarifa ya ujio wa Salma jijini Dar es Salaam, kwa maelezo kuwa alitaka kujiweka salama.
“Tuliwasiliana naye muda mfupi kabla ya kupotea kwake, lakini baada ya hapo hatukuweza kumpata tena. Lakini viongozi wote wa vyombo vya usalama wana taarifa juu ya suala hili,” alisema Olengurumwa. Alisema iwapo hatapatikana kwa siku mbili, wanaweza kufungua kesi mahakamani kuitaka Serikali ihakikishe anapatikana.
Hata hivyo, juzi Salma aliwasiliana na kituo cha Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW) akieleza kuwa alichukuliwa na watu wasiojulikana baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam na kumpeleka asipopajua.
Pamoja na hayo Khamis amekuwa akiwasaliana na mkewe bila ya kujua alipo.
Wadau wa habari walaani
Wadau wa habari nchini wamelaani kitendo cha kutekwa na kupelekwa kusikojulikana kwa mwandishi huyo, wakisema hali hiyo imesababisha fadhaa na mshtuko kwa waandishi, jamii na familia yake hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa marudio Zanzibar.
Katika tamko la pamoja lililotolewa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa-Tanzania), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Umoja wa Klabu za Wanahabari na THRDC, wadau hao wameiomba Serikali kufanya kila linalowezekana kuhakikisha mwandishi huyo anapatikana.
“Taarifa tulizo nazo ni kuwa Salma alishafikisha taarifa Polisi. Kitendo alichofanyiwa mwanahabari huyu ni kibaya, kinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu, lakini pia kinabinya uhuru wa wanahabari na haki ya kupata habari,” alisema Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga.
“Hadi sasa hatujui madhila anayopata Salma na hatujui yupo katika hali gani. Kitendo hiki kinajenga hofu kubwa miongoni mwa wanahabari na jamii kwa ujumla.”
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema taarifa ambayo Salma aliitoa kwa mumewe inaonyesha kukamatwa kwake kunahusiana moja kwa moja na utendaji kazi wake, hususan katika kuripoti habari za uchaguzi wa Zanzibar
“Lakini hata hivyo, kwa sasa ni vyema tukaviachia vyombo vya usalama vifanye kazi yake” alisema Makunga.

 0.2k
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Utata watanda kutoweka kwa mwandishi, wadau walaani Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top