SIMBA SC imepaa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa pointi saba zaidi ya wapinzani Azam na Yanga katika mbio za ubingwa, kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
Simba SC sasa inafikisha pointi 57, baada ya kucheza mechi 24, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 50 sawa na Azam FC baada ya timu zote hizo kucheza mechi 21.
Coastal Union iliyozifunga Yanga 2-0 na Azam 1-0 Uwanja wa Mkwakwani, kipigo cha leo kinawafanya wabaki na pointi zao 19 baada ya kucheza mechi 24 na kuendelea kuburuza mkia katika Ligi Kuu ya timu 16.
Mkali wao; Hamisi Kiiza ameifungia Simba ikishinda 2-0 leo dhidi ya Coastal |
Mshambuliaji Daniel Lyanga aliifunga timu yake zamani dakika ya 39 kuipatia Simba bao la kwanza kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Hamisi Kiiza ‘Diego’ akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 52 akimalizia krosi ya beki wa kulia, Emery Nimubona.
Simba SC ingeweza kuondoka na ushindi mnono zaidi kama washambuliaji wake Kiiza na Lyanga wangetumia vizuri nafasi zaidi walizopata.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohamed Hussein, Juuko Murshid, Novarty Lufunga, Justice Majabvi, Jonas Mkude, Said Ndemla/Awadh Juma dk74, Mwinyi Kazimoto/Mgosi dk87, Hamisi Kiiza na Daniel Lyanga.
Coastal Union; Fikirini Bakari, Hamad Juma, Adeyum Saleh, Hamisi Mbwana, Yusuph Sabo, Yusuph Chuma, Juma Mahadhi, Abdulhalim Humud, Ismail Mohamed/Abasarim Chidiebele dk46, Ally Ahmed ‘Shiboli’/Said Jeillan dk74 na Ibrahim Twaha ‘Messi’/Ayoub Yahya dk46.
0 maoni:
Chapisha Maoni