HALMASHAURI ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora inatarajiwa kukusanya jumla ya shilingi 40,324,170,000/= kutoka katika vyanzo vyake vya ndani,ruzuku kutoka serikali kuu pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora,Bi Rustica Turuka katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na mweka hazina wa Halmashauri ya wilaya,Bwana Gordon Julius Dinda kwenye kikao maalumu cha bajeti cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Aidha Mkurugenzi mtendaji huyo ameweka bayana kwamba taarifa ya mapendekezo ya mpango na bajeti ya Halmashauri ya Igunga ya mwaka 2016/2017 yameandaliwa kwa kuzingatia mwongozo wa uandaaji wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo kutokana na vyanzo vya ndani,Halmashauri inakisia kukusanya jumla ya shilingi 2,678,218,000/= ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 11.84 ikilinganishwa na makisio ya mwaka 2015/2016.
Kuhusu matumizi ya makusanyo hayo,Bi Turuka amebainisha kuwa jumla ya shilingi 29,913,325,000/= ambazo ni sawa na asilimia 74.18 zinatarajiwa kutumika kulipa mishahara ya watumishi,wakati shilingi 3,721,909,000/= sawa na asilimia 9.23 zinatarajiwa kutumika katika matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo zinatarajiwa kutumika shilingi 6,688,936,000/= sawa na asilimia 16.59.
Amesema Halmashauri hiyo inatarajia kupokea kutoka kwa wadau wa maendeleo shilingi 1,745,787,000/=kutoka Mfuko wa pamoja wa Afya,shilingi 622,971,000/=,Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) shilingi 55,914,000/=,Mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Maji shilingi 878,652,000/=,Mradi wa Usafi Binafsi (WASH) shilingi 54,000,000/= na Mfuko wa Umwagiliaji wilaya (DIDF) shilingi 134,250,000/= na hivyo kufanya jumla ya shilingi 1,745,787,000/=
Na,Jumbe Ismailly,Igunga Feb,19,2016 .
0 maoni:
Chapisha Maoni