KAMA ilivyotarajiwa, jana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeongeza idadi ya wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kutoka watano hadi saba kuanzia msimu ujao.
Azimio hilo lilifikiwa jana katika katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika kuanzia Saa 3:00 asubuhi hadi Saa 11:30, ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo, eneo la Kikwajuni, Zanzibar.
TFF imeamua, kila klabu itakayosajili mchezaji wa kigeni imlipie ada ya dola za Kimarekani 2,000 zaidi ya Sh. Milioni 4 za Tanzania, ambazo zitakwenda kwenye mfuko wa Maendeleo ya Soka ya Vijana.
Hatua hii ni matokeo ya mchakato wa muda mrefu, uliotokana na shinikizo la klabu kubwa tatu nchini, Azam FC, Simba SC na Yanga SC, zote za Dar es Salaam.
Klabu hizo ambazo ndizo zimekuwa zikipokezana tiketi za ushiriki wa michuano ya Afrika- zilileta ushawishi huo kwa madai kwamba zinakosa matokeo mazuri katika michuano ya Afrika kutokana na viwango duni vya wachezaji wa Tanzania.
Vikaja na hoja kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuna vipaji vingi, lakini TP Mazembe ya Lubumbashi imesheni wageni na hiyo ndiyo siri ya mafanikio yake.
Na ni kweli, Mazembe wanaweza kupanga kikosi kizima cha wachezaji wa kigeni- ni kweli pia hiyo ni miongoni mwa timu tishio kwa sasa barani.
Mwezi uliopita hoja hiyo ikapenya katika Kamati ya Utendaji ya TFF na ikajadiliwa, kisha yakatolewa maagizo, Kurugenzi ya Ufundi ipitie mapendekezo ya klabu kuhusu wachezaji wa kigeni, baadaye iyawasilishe Kamati ya Mashindano.
Mapendekezo ya jumla ya klabu ilikuwa ni kuwa na wachezaji 10 wa kigeni, lakini Kurugenzi ya Ufundi ikayachuja na kubakiza saba, ambayo bahati nzuri yamepita hivyo hivyo licha ya kupitia Kamati ya Mashindano na baadaye Kamati ya Utendaji.
Tumejimaliza. Yametimia na bila shaka sasa viongozi wa klabu vigogo nchini wanachekelea msimu ujao watasajili wachezaji saba wa kigeni.
Maana yake tarajia katika vikosi vya kwanza vya Azam FC, Simba SC na Yanga SC ambazo kwa muda zimekuwa tegemeo la kutoa wachezaji wa timu ya taifa, kutakuwa na Watanzania 12 tu, wanne kila timu.
Kwa kuwa hizo ndizo timu ambazo kwanza zinalea vizuri wachezaji ukilinganisha na timu nyingine za hapa nchini, kwa kuwalipa vizuri, kuajiri makocha wa kigeni, kucheza mashindano mengi yakiwemo ya Afrika- wazi hili ni pigo kwa timu ya taifa na pigo kwa soka ya Tanzania.
Tumekuwa tunapiga kelele tu, kwa nini wachezaji hawaitwi timu ya taifa hadi wafike Azam FC, Simba au Yanga SC, lakini tunasahau kwamba klabu hizo zina vitu vya ziada ambavyo wachezaji wanapata.
Mwagane Yeya amekuwa tishio kule Mbeya City akapigiwa debe aitwe Taifa Stars na akaitwa tangu enzi za Kim Poulsen, lakini akatemwa. Kadhalika na Mart Nooij alimuita, lakini sasa ameachana naye.
Deus Kaseke na Malimi Busungu waliosajiliwa Yanga SC kutoka Mbeya City na Mgambo JKT, walichukuliwa katika timu ya pili ya taifa iliyokwenda kucheza mchezo wa kirafiki na Rwanda hivi karibuni, lakini baada ya mchezo huo wakatemwa.
Ila kama wachezaji hao watapata nafasi ya kucheza Yanga SC, tarajia kabisa baadaye watakuwa wachezaji wa kudumu wa Taifa Stars.
Napata shaka sana kama watapata nafasi ya kucheza iwapo Yanga SC wataitumia vizuri fursa ya kusajili wachezaji wa kigeni. Saba ni wengi mno.
Katika kikosi cha kwanza cha Azam, Simba au Yanga kutakuwa na wazawa wanne tu! Hii ni hatari kwa kweli na sijui ni wapi soka yetu inaelekea.
Hili ni shinikizo la klabu ambazo bahati mbaya viongozi wake wapo hadi ndani ya Kamati ya Utendaji ya TFF. Wamefikiria maslahi ya klabu zao, wakasahu kabisa kuhusu uzalendo wa taifa lao.
Ni hawa viongozi wa klabu ambao wameshindwa kuzifanya klabu japo ziwe na viwanja vya mazoezi tu, leo wanatuingiza katika janga lingine. Wakati ‘waheshimiwa’ Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF wanatoka kwenye kikao chao jana majengo ya Baraza la Wawakilishi ya zamani eneo la Kikwajuni huku wakichekelea kumaliza kikao salama, niliwatazama kwa jicho la huzuni.
Nilifuata habari, ilinilazimu kuuficha udhaifu wangu na kupata habari kwanza. Lakini nguvu ziliniisha na nikaandika habari ‘bora liende’.
Hiki ni kifo cha soka yetu. Sijui kama hawa watu wanajua. Huwezi kujinafananisha na DRC ambayo ina mamia ya wachezaji wanaofanya vizuri katika Ligi za Ulaya.
Wewe Mtanzania na hao Mbwana Samatta wako na Thomas Ulimwengu wanaocheza DRC, unaweka wachezaji saba kwenye kikosi chako, tena wacheze wote kwa wakati mmoja. Ni mbaya sana.
Tafadhali, kama hawa waheshimiwa watanielewa, nawaomba japo waifanyie marekebisho madogo kanuni hiyo, katika hao wachezaji saba, basi angalau wacheze watano tu kwa wakati mmoja, ili vijana wetu sita wapate nafasi kikosi cha kwanza, ambayo itatusaidia japo kuwa na wachezaji 18 kutoka, Azam FC, Simba na Yanga SC.
Najua, Malinzi amezidiwa na watu waliowakilisha maslahi ya klabu katika kikao cha jana na akaheshimu maamuzi ya kikao, lakini ajue mwisho wa siku jina lake ndilo litatangulizwa kwa lawama zote iwapo hali itakuwa mbaya zaidi katika soka ya nchi hii.
Sijui niandike nini ili Watanzania wenzangu waweze kunielewa. Kwa sasa, tunalia tuna timu dhaifu, yenye wachezaji wenye uzoefu wa kucheza na timu kubwa kama El Merreikh, Etoile du Sahel, Al Ahly na nyingine- je kesho tutakapokuwa na Taifa Stars yenye wachezaji wengi wasio na uzoefu huo tutarajie nini?
Azimio la Kamati ya Utendaji ya TFF Zanzibar jana ni sumu itakayoiua haraka soka yetu. Wakubwa wametumaliza.
Jumanne, 23 Juni 2015
- Blogger Comments
- Facebook Comments
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
0 maoni:
Chapisha Maoni