BAADA YA KUCHABANGWA 2-0 NA WAKATA MIWA, MARCIO MAXIMO ATOA KAULI
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
YANGA
SC imeanza vibaya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015 baada
ya jana kukubali kipigo cha 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyopigwa
uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro dhidi ya wenyeji Mtibwa Sugar.
Ikicheza
mbele ya mashabiki waliofurika kutoka Dar es salaam, Morogoro na mikoa
ya jirani, Yanga ilionesha kandanda safi na kupata nafasi nyingi za
kufunga, lakini washambuliaji wake walichemsha kuzibadili kuwa magoli.
Yanga
walicheza mpira mwingi zaidi kipindi cha pili, wakifika golini kwa
Mtibwa Sugar, lakini walijikuta wakifungwa magoli mawili kwa staili ya
mipira mirefu.
Mussa
Hassan Mgosi katika dakika ya 15 kipindi cha kwanza aliwainua mashabiki
wa Mtibwa akifunga bao la kuongoza kufuatia mabeki wa Yanga, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani kushindwa kuosha mpira mrefu
uliopigwa langoni mwao.
Yanga
waliongoza kumiliki mpira kipindi cha pili, waliikalia barabara Mtibwa
na kukaa langoni kwao kwa muda mrefu, huku Mrisho Ngassa na Saimon Msuva
wakitumia kasi yao kutokea pembeni na kuwahenyesha mabeki wa timu
pinzani.
Wakiwa
na matumaini makubwa ya kusawazisha na kuongeza bao la ushindi, Dakika
ya 83, Ame Ali alipata mpira mrefu na kusumbuana na Cannavaro akiwa na
mwenzake Yondani, akatishia akapiga mpira wa juu ambapo kipa Dida
alipaa juu na kujaribu kuokoa, lakini ukazama nyavuni na kuiandikia
Mtibwa bao la pili.
Goli
hilo lilitokana na uzembe wa mabeki wa Yanga ambapo kwa muda mrefu timu
yao ilikuwa ikishambulia na mpira ulipopigwa hawakuwa tayari
kukuabiliana na shambulizi hilo la kushitukiza.
Baada ya mechi hiyo, watu wengi walitamani kusikia nini atasema kocha mkuu wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo.
Maximo
alisema : “Tulicheza mpira na tukafungwa, lakini ligi ndio inaanza.
Ninachopenda kusema ni kwamba sio vizuri kupoteza matumaini kwasababu
mechi ijayo tutaweza kuimarika na kushinda”
“Tulipoteza
nafasi nyingi, mechi ilikuwa ngumu. Walitumia nafasi zao, sisi
hatukutumia nafasi zetu, ni rahisi tu, mpira wa miguu uko hivyo.
Ukipoteza nafasi unahatarisha vitu vingi”
“Kitu
cha msingi ni kwamba , kamwe timu haitakata tamaa , huo ndio mpira,
wakati fulani siku inakuwa nzuri na siku nyingine inakuwa mbaya”.
Yanga
watacheza mechi ya raundi ya pili septemba 28 mwaka huu uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam dhidi ya Tanzania Prisons iliyoshinda jana mabao
2-0 dhidi ya Ruvu Shootings uwanja wa mabatini, Mlandizi, Mkoani Pwani.
0 maoni:
Chapisha Maoni