Arsenal kuwekeza Bongo
ARSENAL inayoshiriki Ligi Kuu England, imeanza mkakati wa kujikita katika kutafuta ubia na kampuni za Tanzania kwa lengo la kujitangaza na kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii.Katika ziara ya Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Peter Kallaghe, aliyoifanya mapema juma hili katika Uwanja wa Emirates na kufuatiwa na mazungumzo na maofisa wa klabu hiyo, maofisa hao walieleza kutambua umuhimu wa Tanzania katika kukua kwa Arsenal.
Ofisa Miradi ya Jamii, Samir Singh, alimweleza balozi huyo baadhi ya takwimu za mashabiki wa Arsenal waliopo Tanzania, akisema kuwa mtandao wa www.arsenal.com unasomwa na watu zaidi ya milioni mbili kutoka Tanzania, huku wakirudia kuutembelea zaidi ya mara 700,000.
Katika Facebook alisema inafuatwa na watu zaidi ya 120,000.
Pia alisema Arsenal imekuwa ikitoa msaada na makocha kwa mradi wa Tanzania Street Children uliopo Mwanza kwa miaka minne sasa, ambapo kupitia mradi huu watoto zaidi 1,280 wamenufaika.
Naye Ofisa Masoko wa Arsenal, Daniel Willey, alisisitiza umuhimu wa wanachama na wapenzi wa Arsenal kujisajili na kuwa na uongozi imara utakaotambuliwa na klabu ili kupata fursa mbalimbali.
“Umoja wa wanachama unaotambuliwa kutoka huko kwa sasa ni ule wa Kasulu, Kigoma, tuna wapenzi 150,000 na tuna imani wapo zaidi, tunataka tufanye nao kazi. Nitaenda Tanzania hivi karibuni, nitapenda kuonana nao Dar es Salaam, sitakuwa na nafasi ya kwenda nje ya Dar,” alisema Willey.
Kwa upande wake, Balozi Kallaghe, alisema hiyo ni fursa muhimu kwa wapenzi na mashabiki wa Arsenal kuichangamkia.
0 maoni:
Chapisha Maoni