Chelsea wazidi kupaa Ligi Kuu
Chelsea wametengeneza pengo la pointi saba kileleni mwa Ligi Kuu ya England (EPL) wakati Arsenal wakiingia nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA.Chelsea walikwaruzana na timu ngumu ya Tottenham Hotspur na katika kipindi cha kwanza mambo yalikuwa doro lakini yakabadilika na kuwa moto kipindi cha pili.
Mabao yote manne yalipatikana kwenye nusu ya pili, la kwanza likitokana na makosa ya beki Jan Vertonghen dakika ya 56 aliyemwachia Samuel Eto’o kucheka na nyavu na kushangilia kwa aina yake akishika kibendera cha kona mkono mmoja na mwingine kiunoni.
Dakika nne baadaye majanga yaliendelea, kwa Younes Kaboul kumchezea rafu Eto’o, mchezaji huyo wa Spurs akatolewa nje kwa kadi nyekundu na Eden Hazard akafunga penati iliyotolewa kama adhabu kwa kosa hilo.
Demba Ba alifunga bao la tatu dakika ya 88 kutokana na makosa ya Sandro, kabla hajaamsha tena mashabiki kwa kupachika la nne dakika moja tu baadaye, akinasa mpira wa kichwa uliorudishwa nyuma na beki wa Spurs, Kyle Walker.
ARSENAL WAWATUPA NJE EVERTON
Arsenal wameendeleza vyema kampeni yake ya kuwania mataji msimu huu kwa ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Everton katika dimba la Emirates.
Mesut Ozil ambaye amekuwa akilaumiwa kwa kucheza chini ya kiwango ndiye aliyepachika bao la kuongoza dakika ya saba tu ya mchezo kabla ya Romelu Lukaku kusawazisha dakika ya 32 na timu kwenda mapumziko zikiwa sare.
Mikel Arteta alifunga bao la pili kwa penati dakika ya 68 kutokana na Gareth Barry kumchezea faulo ya kijinga winga Alex Oxlade-Chamberlain.
Arsenal walielekea kuumiliki mchezo vyema na Olivier Giroud aliyeingia badala ya Mfaransa mwenzake, Yaya Sanogo alipachika mabao mawili yaliyopigilia msumari kwenye jeneza la Everton, akipokea mipira ya Bacary Sagna kwa bao la tatu dakika ya 83 na wa Ozil kwa bao la nne dakika mbili tu baadaye.
Kwa ushindi huo Arsenal wanakwenda Wembley kwa ajili ya nusu fainali na watakaopambana nao itategemeana na matokeo ya mechi za robo fainali nyingine Jumapili hii.
Sheffield United wanacheza na Charlton, Hull dhidi ya Sunderland huku Manchester City wakikabiliana na Wigan ambao ni wagumu na walitwaa kombe hili mikononi mwa City hawa hawa, kitendo kilichosababisha kufukuzwa kazi kocha wa City, Roberto Mancini msimu uliopita.
MAN UNITED WAAMKA
Manchester United wamefanikiwa kurudisha matumaini, japo kidogo ya kupata moja ya nafasi nne za juu kwenye EPL, baada ya kuwashinda West Bromwich Albion 3-0 kwao.
West Brom waliwaadhiri United katika dimba la Old Trafford msimu huu na David Moyes na vijana wake walisafiri wakiwa na nia moja ya kupata ushindi na kujaribu kuondokana kwenye matokeo mabaya aliyoanza nayo Mskochi huyo.
Mabao ya United yalifungwa na Phil Jones, Wayne Rooney na Danny Wellbeck na kuwafanya Manchester United kuwa katika nafasi ya saba kwa pointi zake 48 sawa na Everton wanaowafuata wakiwa na mchezo mmoja mkononi wakati vinara Chelsea wanazo 66.
Katika mechi nyingine, Cardiff waliakung’uta Fulham 3-1, Crystal Palace wakalala kwa Southampton 0-1 na Norwich wakaenda sare ya 1-1 na Stoke.
Nafasi ya pili ya ligi inashikiliwa na Liverpool wenye pointi 59 sawa na Arsenal, lakini Liverpool wana uwiano mzuri wa mabao, ya nne ikishikwa na Manchester City wenye mechi mbili mkononi. Liverpool na Arsenal wamecheza mechi moja pungufu ya Chelsea
Everton watinga nne bora
Arsenal safi, Man United hoi
*Arsenal wapeta Kombe la FA
*Man U warudisha matumaini
Chelsea, Man U watesa EPL
0 maoni:
Chapisha Maoni