Mbowe: Muulizeni Zitto nilikomtoa
MWENYETI wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, amewataka
wanachama wa chama hicho wamuulize Mbunge Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe
wapi alikomtoa hadi kufikia ngazi na hadhi aliyonayo sasa katika medani
ya siasa nchini.
Mbowe alitoa
kauli hiyo jana katika kongamano la miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara,
lililoandaliwa na Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Chaso) kwa
kushirikiana na Baraza la Vijana la Chama hicho (BAVICHA)
Katika
kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Land Mark, Mbowe ambaye
alianza kwa kutaja historia yake kama mwasisi kijana wa CHADEMA na
mwenyekiti wa kwanza, alisema mwaka 2003 akiwa katika harakati za
kukijenga chama, alipita katika vyuo mbalimbali ili kupata vijana wasomi
wajiunge na CHADEMA na ndipo alipompata Zitto, akiwa katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam.
“Nikiwa
katika harakati zangu za kukijenga chama, nilipita Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam …nilibahatika kuwapata kina John Mrema, Halima Mdee, Zitto
Kabwe, John Mnyika wakiwa viongozi ambao walipenda siasa ya mabadiliko,
nami nikaondoka nao bila ya kusita,” alisema.
Alisema nia
ya kuwachukua vijana hao ni kujenga chama kama taasisi ili kisonge mbele
tofauti na ilivyo sasa na siyo kujenga jina la mtu kama watu
wanavyotaka iwe au wanavyodhani.
Mbowe
alisema akiwa na vijana hao pamoja na viongozi wengine, walifanya kazi
kama timu ili kuhakikisha wanakiingiza chama hicho Ikulu, akiamini kuwa
asingeliweza peke yake kukipeleka mbele chama hicho.
Aliwataja
viongozi aliowachukua kutoka katika vyama vingine vya siasa kuwa ni
pamoja na Mkurugezi wa Fedha wa chama hicho, Antony Komu, Tundu Lissu,
Mabere Marando ambao walitoka NCCR – Mageuzi.
Wengine ni
Godbless Lema, Saidi Arfi na Mchungaji Peter Msigwa ambao walikuwa TLP
na Ezekia Wenje aliyetoka Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwa mwenyekiti wa
tawi moja la chama hicho huku Mwanza.
Alisema
safari ya kukijenga chama sio lelemama kwani ni sawa na treni inayotoka
Dar es Salaam kuelekekea Kigoma huku akiamini wote watafiki, lakini
imekuwa tofauti kwani wapo walioshuka njiani.
“Safari yetu
ya Kigoma toka Dar es Salaam ilikuwa ndefu sana … wapo walioshuka
katika kituo cha kwanza tu Pugu, wengine Morogogo na vituo vingine
vilivyofuata na kupata vilevile lakini tutafika tu,” alisema.
Akitoa
historia fupi ya maisha yake katika siasa, Mbowe alisema aliingia akiwa
kijana mdogo muasisi ambaye alipata nafasi ya kukiongoza chama kama
mwenyekiti wa kwanza wa vijana, baadaye kupata nafasi mbalimbali ikiwamo
uenyekiti.
Alisema
aliingia katika chama hicho na kuchanguliwa kuwa kiongozi, lengo likiwa
kufanya mabadiliko kwa vitendo na si kwenda kupata faida kama watu
wengine wanavyofikiria.
“Lakini
nilifanya kazi yangu ya kuijenga CHADEMA hatua kwa hatua kwa maana
nyingine nimefanya kazi ya chama kwa miaka 23 sasa bila kulipwa mshahara
wowote kwa sababu mimi ni mfanyabiashara,” alisema.
Alisema chama akitatoa maamuzi ya kumwonea mtu yeyote bali kitamhukumu mtu kutokana na makosa yake.
Dk. Slaa aitikisa Kigoma
Wakati
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa akiwasili mjini Kigoma kwa ziara ya kukagua na kuimarisha
uhai wa chama, hali ya ulinzi katika mikutano imeimarishwa kwa ajili ya
kudhibiti vurugu zinazopenyezwa na watu wanaotumia jina la Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Dk. Slaa
alipata mapokezi mazito akiwa na msafara wa magari zaidi ya 22, pikipiki
150, magari manne ya polisi na ulinzi umeimarishwa mara dufu.
Kabla ya
kuwasili mjini Kigoma, Dk. Slaa alifanya mkutano katika eneo la Janda na
Mnanila, katika Jimbo la Manyovu, Wilaya ya Buhingwe, ikiwa ni siku
yake ya tano tangu aingie mkoa wa Kigoma, akitokea Shinyanga.
Dk. Slaa
alihoji matunda ya uhuru ‘kumilikiwa’ na kikundi kidogo cha watu
wanaotumia dhamana za uongozi kufanya ufisadi unaoangamiza matumaini ya
Watanzania.
Alisema kuwa
wakati nchi ikifikisha miaka 52 tangu kupata uhuru Desemba 9, 1961,
Watanzania wengi hawana kitu cha kusherehekea kwa sababu malengo ya
mapambano ya kumwondoa mkoloni yamefifishwa na watu walioko kwenye
dhamana ya uongozi, kiasi kwamba hata maadui waliotangazwa wakati wa
uhuru badala ya kupungua, wameongezeka.
“Ndugu zangu
hata ninyi hapa mmekubali kuwa miaka 52 baada ya uhuru maadui
wameongezeka na bila woga mmesema ufisadi ni adui aliyeongezeka. Hivyo
katika wale maadui watatu wa taifa waliotangazwa na Mwalimu Julius
Nyerere kuwa tunapaswa kupambana nao na kuwatokomeza, yaani ujinga,
maradhi na umaskini, ameongezeka adui ufisadi.
“Yaani
hatujamalizana na ujinga, hatujamalizana na umaskini, hatujamalizana na
maradhi, viongozi wetu kutokana na ulafi na ubinafsi wao, wametuongezea
adui ufisadi.
“Huyu sasa
amekuwa ndiye msingi wa maadui wote, adui umaskini anasaidiwa kuendelea
kwa sababu ya ufisadi, adui ujinga anasaidiwa kuishi kwa sababu ya
ufisadi, halikadhalika adui maradhi,” alisema Dk. Slaa kijijini Janda.
Dk. Slaa
aliyewasili jimbo la Manyovu akitokea jimbo la Kasulu mjini, alisema
kuwa miaka 52 baada ya uhuru Watanzania waliokuwa na matumaini ya
kujitawala, hawana uhakika wa kusherehekea kwa sababu madhira
wanayokabiliana nayo sasa mengine hata wakoloni hawakufanya kwa raia.
“Wananchi
wenzangu wa Mnanila, wazee wetu hawakupambana kumwondoa mkoloni
Mwingereza kwa sababu ya rangi yake, ilikuwa ni kwa sababu waliona wazi
kabisa kuwa alikuwa ameshindwa kuondoa umaskini, ameshindwa kuondoa
ujinga, ameshindwa kuondoa maradhi.
“Ndiyo maana tunasema tunahitaji kuunga mkono vuguvugu la mabadiliko ya kumwondoa mkoloni mweusi ambaye ni CCM.
“Hatuwaondoi
CCM kwa sababu ya rangi, kabila, dini wala chochote kile cha namna
hiyo. Ni kwa sababu miaka 52 baada ya uhuru tunaona kabisa wameshindwa
kutuongoza, wamevuruga hata misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa
wakiongozwa na Mwalimu Nyerere. Wamevuruga hata tunu tulizojengewa kwa
muda mrefu,” alisema Dk. Slaa.
Hali ya ulinzi
Wakati
mikutano ya Dk. Slaa ikiendelea na kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na
chama hicho, leo ataingia jimbo la Uvinza, hali ya ulinzi imeonekana
kuimarishwa ambapo gazeti hili jana lilishuhudia idadi kubwa ya askari
polisi takriban 50, katika eneo la Mnanila, wakisimamia ulinzi na
usalama.
Gazeti hili
limedokezwa kuwa hali hiyo inatokana na chama hicho kubaini na kutoa
taarifa hadharani, huku pia kukiwa kuna mikakati inayopangwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni