
SIRI nzito imefichuka kuwa miongoni
mwa walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi yumo mmoja wa wanasiasa maarufu
anayetajwa kuwa anataka kuwania urais mwaka 2015. Sakata la mabilioni ya
fedha za Tanzania kufichwa nchini Uswisi liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), ambapo kwa sasa yupo nchini humo kwa ajili ya
kufuatilia kwa kina fedha hizo na waliozificha. Hata hivyo, kutokana na
uzito wa suala hilo, Kamati
Maalumu ya Bunge imepewa jukumu la
kufuatilia fedha hizo ambazo baada ya kubainika kufichwa ziliibua mjadala
mkubwa nchini huku wanasiasa kadhaa wakitaka walioficha watajwe hadharani na ikiwezekana
zitaifishwe. Taarifa ambazo Jambo Leo imezipata zinaeleza kuwa miongoni
mwa majina ya watu ambao wanadaiwa kuweka fedha hizo yumo mwanasiasa maarufu
anayetajwa kuwania urais (jina tunalo). “Tuna taarifa za uhakika kuwa
mmoja wa
wanasiasa anayetajwa kutaka kuwania
urais mwaka 2015 naye anahusishwa kuwa ameficha fedha
Uswisi. Tunaamini Zitto
atakuja na ukweli maana analifuatilia kwa karibu,” kilidokeza chanzo chetu cha
habari.
Hata hivyo, Zitto wakati
anazungumzia suala hilo kabla ya kuondoka kwenda Uswisi alisema
Watanzania watafahamu ukweli kuhusu fedha hizo kuanzia walioficha majina na
akaunti zao. Akitoa maoni yake kuhusu mabilioni ya fedha za Tanzania
kufichwa nchini Uswisi, Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF),
alisema ni vema ikafahamika mtu au mfanyabiashara kuweka fedha nje ya nchi yake
si kosa. Alifafanua kuwa kosa linaweza kujitokeza iwapo katika kuweka
fedha hizo taratibu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo huidhinisha suala
hilo haukufuatwa. “Mfanyabiashara au mtu yeyote anaweza kuweka fedha nje kama
amekubaliwa na taratibu husika za BoT.
“Kama amekubaliwa hakuna pingamizi
na atakuwa huru kuweka fedha zake, katika hilo hawezi kupata msukosuko kwani
kila kipengele ametimiza kikiwemo cha kukatwa kodi halali ya fedha hizo,”
alisema.
Hata hivyo, alisema fedha hizo
ambazo zinadaiwa kufichwa nchini Uswisi zinaweza kuwa na mambo makubwa mawili,
moja zimefuata utaratibu au kutofuata taratibu za BoT.
“Inawezeka kuna ajenda nyingine ya
fedha hizo kufichwa kwa sababu tu ya kutaka kukwepa kulipa kodi halali na
kujipatia fedha kwa njia isiyokuwa sahihi,” alisisitiza.
Pia alisema inawezekana sababu
nyingine ya kuficha fedha hizo ni kwamba zimepatikana kwa njia haramu
ikiwemo ya biashara ya dawa za kulevya au kamisheni iliyotokana na njia isiyo
halali na kufanya wenye fedha hizo kuzifichwa nje ya Tanzania.
Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa jina
la mwanasiasa anayetaka kuwania urais mwaka 2015 kuwa anadaiwa kuweka fedha
Uswis akishirikiana na wenzake, alijibu kuwa katika maisha yake haamini habari
za kusikia bali anataka habari ambazo zimethibitishwa.
“Niwaombe Watanzania wenzangu kuwa
hakuna sababu ya kuishi kwa kusikia habari za fununu, ni vema mkafanyakazi kwa
taarifa za uthibitisho. Siku hizi imekuwa ni mambo ya kawaida watu kushutumiana
na kuchafuana kwa kutaja majina ya watu bila ushahidi.
“Hili si jambo nzuri tunapaswa
kubadilika. Ni dhambi hata kwa Mwenyezi Mungu kumshutumu mtu bila sababu,”
alisema.
Kuhusu sakata hilo, alisema Bunge
liliunda kamati ya kuchunguza suala hilo na bado inamalizia kazi hiyo na kwamba
ripoti yake itakabidhiwa katika vikao vijavyo vya Bunge, hivyo ni vema
Watanzania wakawa na subira na si kuanza kutajana majina kwa lengo la
kuchafuana.
“Nimefurahishwa na juhudi
zinazofanywa na Zitto kuhusu ya jambo hilo na ninaamini kwa vile ni miongoni
mwa watu wanaolichunguza atakuja na majina ya watu waliotorosha fedha hizo nje
ya nchi na kuwataka Watanzania wasubiri,” alisema.
Pia alisema kama ni kweli anayetajwa
ni mgombea urais mtarajiwa basi sifa zake zitaishia hapo kwani hata baba wa
taifa aliwahi kusema mtu anayetumia fedha kuingia Ikulu atakuwa amezipata wapi
na atazirudishaje. Mwenyekiti wa Demokratic Party (DP), Mchungaji
Christopher Mtikila alisema haamini kama Zitto anaweza kuwa na majibu sahihi maana
hao hao ambao wameficha fedha ana maslahi nao kisiasa.
“Pamoja na porojo na propaganda
zinazotolewa na Zitto jibu atakalokuja nalo baada ya kutoka Uswisi halitakuwa
na mshiko kutokana na yeye kuwa na maslahi tofauti na watu wanavyofikiri,”
alisema Mtikila.
Hata hivyo, Zitto amekuwa
akizungumzia msimamo wake kuwa atahakikisha analisimamia na
Watanzania watapata
ukweli na kamwe hatayumbishwa na mtu yeyote katika suala hilo. Kabla ya
kuondoka mwishoni mwa wiki iliyopita kwenda Uswisi, Zitto aliwataka Watanzania
wamuamini kwani anakwenda kutafuta ukweli na wote ambao watakaohusika majina
yao atayaanika hadharani.
0 maoni:
Chapisha Maoni