Kaze raia wa Burundi aliyezaliwa Januari 25, 1992 ambaye amejiunga
na Simba msimu huu akitokea Vital’O ya Burundi, aliifungia Simba bao la tatu na
kuisawazishia klabu yake dakika ya 83 kufanya matokeo kuwa mabao 3-3.
Katika mahojiano yake muda mfupi baada ya mchezo huo, Kaze beki
mrefu mwembamba anayezungumza kwa taratibu, aliuambia mtandao huu kwamba,
anajisikia fahari kufunga bao hilo na kuifanya timu yake kupata matokeo ya sare
wakitoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa mabao 3-0.
“Sikujua kama nitafunga bao, lakini nikauona mpira upo peke yake
nami nikajituma na kuuwahi mpira wa faulo uliopigwa na Chollo, nashukuru
kufunga bao langu la kwanza katika ligi hii pia kuifunga Yanga timu ambayo ni
pinzani na hii ninayoichezea.
“Nashukuru jinsi mashabiki wa Simba walivyotuvumilia wakati
tulipokuwa nyuma kwa bao 3-0 na hata makocha walifanya kazi nzuri ya kutuweka
sawa kisaikolojia wakati wa mapumziko na tukaweza kufanya vizuri na kusawazisha
mabao yote,” anasema Kaze.
Kuhusu ligi kuu ya bara...
Kaze anasema Ligi Kuu ya Bara ni ngumu kuliko ligi ya Burundi
aliyoichezea msimu uliopita na kukiri kila timu anayokutana nayo ni nzuri na
inayoonekana imejiandaa kwa kucheza ligi.
Anasema kila mechi alizocheza katika ligi kuu ya bara anakutana na
washambuliaji na viungo hatari na wenye nguvu nyingi hivyo analazimika kutumia
nguvu nyingi na yeye wakati mwingine ili aweze kuendana na wapinzani wake.
“Unajua ligi hii ya Tanzania ni ngumu kulinganisha na ile ya
Burundi niliyocheza msimu uliopita, hapa kila timu inaonekana imejiandaa
kupambana na sioni kama wanakamia bali ndivyo wanavyocheza na ndiyo maana hata
wakati mwingine tunashinda kwa taabu sana,” anasema Kaze.
Vipi anaonekana hana nguvu uwanjani..
Katika mechi nyingi alizoichezea Simba, Kaze amekuwa akionekana
kama mchezaji asiye na nguvu na kushawishi washambuliaji wa timu pinzani
‘kumtamani’ na kumfuata kutaka kupambana naye tofauti na beki mwenzake Joseph
Owino.
Lakini mwenyewe anakiri kuwepo kwa hali hiyo lakini anawataka wadau
wa soka kutofautisha nguvu na kucheza polepole, kwani yeye hachezi kwa kasi
sana kulingana na aina ya wachezaji au timu pinzani anayocheza nayo.
“Naweza kuonekana sina nguvu, lakini si kweli. Unajua hata Ulaya si
kweli kwamba wachezaji wote wana nguvu sawa. Sasa kama naonekana nina nguvu
kidogo hicho ni kitu cha kawaida kwani pamoja na hali hiyo mbona nacheza na
kocha anashukuru kwa kazi yangu.
“Mimi wakati fulani huwa nacheza taratibu kutegemea na mchezo
ulivyo, huwezi kucheza kwa papara mbele ya wapinzani wenye akili ya mpira na
nguvu pia. Kuna wakati beki unatakiwa kucheza kwa akili zaidi kuliko nguvu,”
anasema Kaze.
‘Partinership’ yake na Owino
Katika kikosi cha Yanga, nafasi ya beki wa kati wapo Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani, hawa wamecheza muda mrefu na wanamudu kucheza
sambamba ndani ya kikosi cha Yanga na wakati mwingine katika timu ya taifa ya
Tanzania, Taifa Stars.
Hata Arsenal kwa sasa wapo Per Mertesacker na Laurent Koscielny,
ukienda Manchester United utakutana na Nemanja Vidic na Rio Ferdinand, ndani ya
kikosi cha Simba kwa sasa wapo Kaze na Joseph Owino.
Tofauti na safu zote hizo, Kaze na Owino wanaonekana hawaelewani na
pia wanacheza bila kuwasiliana na ndiyo maana wanaruhusu mabao mengi rahisi, lakini
Kaze anasema ni hali ya kimchezo tu inayofanya wafungwe na siyo kutoelewana
kwao.
“Ukuta wetu ni mpya, nasi hatujakaa kwa muda mrefu na ndiyo maana
hadi leo tunacheza. Tatizo langu lililokuwepo ni kutokaa pamoja kwa muda mrefu
lakini nadhani si tatizo sana kwetu,” anasema Kaze.
0 maoni:
Chapisha Maoni