Jumatatu, 17 Februari 2014



SINGIDA
Mkazi wa mtaa wa mahembe kata ya kindai Bw Daudi Saimoni  amejeruhiwa na watu wasiojulikana kwa kupingwa risasi kwenye nyonga upande wa kulia

Kamanda wa polisi mkoani Singida Bw Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea leo alfajiri

Amesema tukio hilo limetokea wakati Bw. Saimon  akiwa amelala nyumbani kwake ambapo ilipofika saa 9:00 alfajiri  watu hao walifika katika nyumba hiyo na kufungua dirisha na kisha kumpiga Risasi huku wakimtaka kutoa mali

Majeruhi amelazwa katika hospitali ya mkoa wa singida na hadi sasa hakuna mtu anaeshikiliwa kutokana na tukio hilo.



SINGIDA
Mahakama  ya  mwanzo  ya  utemini  imehamishia  kesi  katika  Mahakama  ya  wilaya  ya  singida  inayo mkabili  Bw Sebastiani  John  kwa tuhuma za  kumtorosha  mshitakiwa

Akihamisha kesi  hiyo Hakimu Fedinarnd Njau amesema mshitakiwa   alimdhamini Bw Fredy Mawala kwa kuahidi shilingi laki moja ambaye alikuwa akikabiliwa na shitaka la kukataa kuchangia ujenzi wa maabara ya sekondari ya  Iglasoni

Mshitakiwa hakutimiza  mashariti  ya dhamana  ya kumfikisha  mtuhumiwa Januari 20 mwaka  huu katika mahakama ya utemini

Hakimu Njau amesema kutokana na mshitakiwa kukubali kosa amesomewa shitaka na  kuomba kuleta wakili katika kesi hiyo ndipo hakimu akaihamisha na kuipeleka mahakama ya wilaya ya Singida kwa kile alichokieleza kuwa mahakama za mwanzo hazisikilizi kesi zinazosimamiwa  na wakili.

Bw  Fredy  Mwela alikuwa akishitakiwa na Afisa mtendaji wa kata ya Igrasoni  Bi  Rehema  Majii kwa  tuhuma za kukutaa kutoa shilingi elfu 20 kwa ajili  ya  ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Igrasoni



DAR ES SALAAM
Serikali  imesema ina mpango wa kuhakikisha Halmashauri zote nchini, zinakusanya mapato kupitia mfumo wa mashine za kielektroniki ifikapo mwaka 2015/16

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bi. Hawa Ghasia, amesema mfumo huo umeanza katika baadhi ya halmashauri ambao umesaidia kuongeza makusanyo ya mwaka.
Amesema lengo la kuweka mashine hizo ni kudhibiti wizi wa fedha za serikali zilizokuwa zinakusanywa kwa njia ya mkono hivyo kuikosesha serikali kiasi kikubwa cha mapato.

Amesema halmashauri ambazo zimeanza kukusanya mapato kutumia mfumo wa elektroniki zimeongeza kipato ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Ameitaja miji inayoongoza kwa kukusanya mapato vizuri kuwa ni jijini Dar es Salaam (Temeke), Arusha, Mwanza, Mbeya na katika Halmashauri ni Msonga, Tandahimba na Misungwi

Amewataja Wakurugenzi 53 waliokamatwa kwa ubadhirifu wa fedha za halmashauri kuwa, mmoja alifukuzwa kazi, sita walisimamishwa, nane wako mahakamani, 12 walipewa onyo, 25 walivuliwa madaraka na mmoja kesi yake ipo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).


TARIME
Watu  wanane wanaodhaiwa kuwa washirika wa mtuhumiwa wa mauaji ya watu kadhaa wilayani Tarime, marehemu Charles Range Kichune, aliyefariki wakati akipatiwa matibabu wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime wakikabiliwa na kesi ya mauaji.

Imedaiwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Tarime, Adrian Kilimi, na Mwendesha Mashitaka, George Lutonjo kuwa, watuhumiwa 10 ni pamoja na  mwendesha pikipiki Marema Mweri Kibwabwa  aliyekuwa akimsafirisha marehemu  wakati wa matukio na kumtorosha hadi Musoma.

Wengine ni Elizabeth  Kitara Mwita, Mairo Chacha Kegoro, Joram Mwita Chacha,  Simion  Marwa Bisumwa, Kyoma Manghu Nyaseba, Chacha Mahegere Bugichere na Yohana Mgosi Kimom.

Amedai kuwa watuhumiwa katika nyakati tofauti kuanzi Januari 26 hadi Januari 28 waliua watu tisa kwa kuwapiga risasi.
Watuhumiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.


DAR ES SALAAM
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo imefanya kikao cha dharura  kujadili na kufanya uteuzi wa jina la mgombea ubunge wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa  wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa.

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kutangaza kuwa uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo utafanyika Machi 16, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari, Chadema kitafanya uteuzi wa mwisho baada ya mchakato wa ndani wa kumpata mgombea ubunge wake wa jimbo hilo kuwa umepitia hatua za awali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,  wanachama wa chama hicho 16 walichukua fomu za kuwania uteuzi huo na kwamba hadi siku ya mwisho,  13 walirejesha kupita kwenye mchakato wa kura za maoni, zilizofanyika Februari 12, mwaka huu.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa kufariki dunia.


DAR ES SALAAM
Serikali itapunguza gharama za kukopa fedha kwa riba katika taasisi za fedha na benki nchini, baada ya Benki ya Rasilimali (TIB) kuingia makubaliano na Benki ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, katika kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa miradi yote ya maendeleo ikiwamo ya sekta ya uchukuzi.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, amesema hayo jana wakati benki hizo mbili ziliposaini mkataba wa ushirikiano mwema wa kuwekeza katika sekta ya uchukuzi.
Amesema kupitia ushirikiano huo, Serikali itapunguza kukopa katika benki na taasisi za fedha zenye riba kubwa na badala yake, itatumia fursa hiyo kukopa kutoka TIB kwa ajili ya miradi yote ya maendeleo ikiwemo miundombinu.
Mkurugenzi Mkuu wa TIB, Peter Noni, amesema kwa kipindi kirefu uongozi wa benki hiyo umekuwa katika majadiliano na DBSA kwa lengo la kupata fedha za kuendeshea miundombinu katika sekta ya uchukuzi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa DBSA, Patrick Dlamini amesema benki hiyo ni taasisi ya kifedha ya Serikali ya Afrika Kusini na kwamba imelenga katika kusaidia miradi mikubwa.


                                HABARI ZA KIMATIFA

KINSHASA
Ujumbe wa Umoja wa mataifa mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, umesema kuwa zaidi ya watu sabini wameuawa mwisho wa mwezi uliopita na mapema mwezi huu.
Afisa mmoja wa shirika la Monusco, mjini Goma, Ray Tores, amesema ndege ya kijeshi iliyokuwa ikifanya uchunguzi, katika eneo hilo iligundua kuwa vijiji vitatu viliteketezwa na kuharibiwa kabisa.
Amesema wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa watatembelea eneo hilo baadaye ili kufanya uchunguzi zaidi.
Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa limeimarisha ulinzi katika eneo hilo, tangu kusambaratishwa kundi la waasi wa M23, Novemba mwaka uliopita.
Bw.  Torres, amesema kuwa zaidi ya makundi arobaini ya waasi yanaendesha operesheni zao katika eneo hilo la Goma.
Manne kati ya makundi hayo yamekuwa yakifanya mashambulio ya mara kwa mara na hivyo kuwa tishio la usalama.


BANGUI
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean – Yves Le Drian akiwa amefuatana na Rais Catherine Samba – Panza wa serikali ya mpito ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wametembelea eneo la Mbaiki, umbali wa kilomita 80 kusini mwa Bangui, mji mkuu wa nchi hiyo.
Hivi karibuni, Ufaransa imekuwa ikizikosoa operesheni zinazofanywa na jeshi la serikali ya Jamhuri ya Afrika ya kati dhidi ya wanamgambo wa Kikristo wa Anti Balaka.
Rais Samba - Panza ametangaza mapambano dhidi ya kundi la Anti Balaka.
Mara baada ya kutokea vitendo vya mauaji, uporaji wa mali za watu vilivyohusishwa na  wanamgambo wa muungano wa Seleka, Michael Djotodia aliyekuwa rais wa serikali ya mpito nchini humo aliuvunja muungano huo kwa lengo la kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Juhudi hizo za Michael Djotodia ambaye alikuwa Muislamu na Nicolas Tiangaye Waziri Mkuu wa serikali ya mpito nchini humo hazikufanikiwa, kwani waliamua kuachia  nyadhifa zao baada ya kukabiliwa na mashinikizo ya wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati kuwataka wajiuzulu.



BRUSSELS
Wabunge Nchini Ubelgiji, wamepitisha sheria inayoruhusu mtoto kufanya maamuuzi kuhusu masuala ya kifo anapokuwa mgonjwa mahututi kupindukia.
Hiyo imeifanya Ubelgiji kuwa taifa la kwanza duniani kupitisha sheria hiyo inayoruhusu mtu kuamua maisha yake kukatizwa kwa hiari yake mwenyewe. .
Licha ya pingamizi kutoka kwa kanisa la katoliki, idadi kubwa ya wabunge wa nchi hiyo wameunga mkono sheria hiyo, iliyoidhinishwa mwaka wa 2002, ambayo iliruhusu watu wazima kuchukua maamuzi kuhusu maisha yao wakiwa katika hali mahututi.
Sheria hiyo inasema kuwa ni sharti mtoto awe katika hali mbaya ya afya na katika hatari ya kufa kutokana na mateso anayopata na pia katika hali nzuri kimawazo ili kuchukua uamuzi huo.
Sasa sheria hiyo itatumika kwa watoto walio katika hatari ya kufa, iwapo watawasihii wazazi wao na madaktari kwamba wanataka kufa kama njia ya kuwaondolea mateso.


NA HAYA NI MACHACHE KATI YHAMENGI AMBAYO UMEYASO LEO .
*Mkazi wa mtaa wa mahembe kata ya kindai Bw Daudi Saimoni  amejeruhiwa na watu wasiojulikana kwa kupingwa risasi kwenye nyonga upande wa kulia
*Watu  wanane wanaodhaiwa kuwa washirika wa mtuhumiwa wa mauaji ya watu kadhaa wilayani Tarime, marehemu Charles Range Kichune, aliyefariki wakati akipatiwa matibabu wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime wakikabiliwa na kesi ya mauaji.
* Ujumbe wa Umoja wa mataifa mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, umesema kuwa zaidi ya watu sabini wameuawa mwisho wa mwezi uliopita na mapema mwezi huu.

* Wabunge Nchini Ubelgiji, wamepitisha sheria inayoruhusu mtoto kufanya maamuuzi kuhusu masuala ya kifo anapokuwa mgonjwa mahututi kupindukia.
HONGERA SANA MTU WANGU WA UKWELI KWA KUSOMA 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top