YANGA YAIKARIBISHA RHINO DAR LEO, SIMBA KAZI IPO MKWAKWANI MBELE YA COASTAL
YANGA
na Simba kwa pamoja leo zinashuka katika viwanja viwili tofauti
kupambana na Rhino Rangers na Coastal Union katika muendelezo wa Ligi
Kuu ya Bara.
Yanga
ambayo ni mabingwa watetezi wenyewe watakuwa jijini Dar es Salaam
kwenye Uwanja wa Taifa, kuvaana na Rhino ya Tabora inayomilikiwa na
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JW).
Kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro amesema vijana wake wamefuta makosa na sasa wapo tayari kuikabiri Rhino Rangers leo.
“Kikosi
kipo sawa kupambana na Rhino hapo kesho (leo), kama ni makosa
tumeshayafanyia kazi na nadhani tutafanya vizuri zaidi katika mchezo huu
na kilichobaki sasa ni muda kufika tuweze kuingia uwanjani,” anasema
Minziro.
Yanga
ilianza mazoezi juzi Jumatatu asubuhi kwenye Uwanja wa Shule ya
Sekondari Loyora jijini Dar es Salaam baada ya Jumapili kutoka sare na
Simba ya mabao 3-3 na Simba kwenye Uwanja wa Taifa.
Hadi
sasa Yanga ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 16 katika michezo 9. Rhino
yenyewe ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 7 katika michezo 9.
NAKO
mjini Tanga, Simba inashuka dimbani leo mchana kupambana na Coastal
Union ya mjini humo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Ofisa
Habari wa Simba, Ezekile Kamwaga ameuambia mtandao huu kwamba, kikosi
cha Simba kiliwasili salama Jumatatu jijini Tanga tayari kwa mchezo huo
wa leo na wachezaji Henry Joseph, Haruna Chanongo na Abdulhalim Humud
hawapo katika kikosi hicho.
“Timu
imefika salama Tanga tangu Jumatatu mchana na hali ya kikosi kizima ni
nzuri kinachosubiriwa sasa ni muda kufika ili tuweze kutazama pambano
hili safi na la kuvutia kwetu sote, kwani Coastal ni timu nzuri ambayo
ina wachezaji kadhaa ambao wamewahi kuwika na klabu mbalimbali za hapa
nchini.
“Sisi
kama Simba tunaamini tuna timu nzuri ambayo inaweza kupambana na timu
yoyote na kutwaa ubingwa hivyo wakazi wa Tanga na miji ya jirani
wajitokeze kwa wingi uwanjani kutazama pambano hili la kuvutia,” anasema
Kamwaga.
Naye
Mwenyekiti wa Coastal, Ahmed Aurora amesema kikosi cha timu yake
kimejiandaa vya kutosha na hakuna tatizo lolote linaloikabiri timu yake
kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Simba.
“Sisi
tupo vizuri kabisa tunaisubiri Simba kwa hamu kubwa kuweza kupambana
nao kwani tumejiandaa vizuri chini ya kocha wetu Joseph Lazaro ambaye
amejiunga nasi hivi karibuni akichukua nafasi ya Ahmed Morocco.
“Tuna
wachezaji wengi wazuri ambao wamewahi kutamba na timu kubwa za Simba,
Yanga na Azam, tunachohitaji sisi ni kufanya vizuri kwenye uwanja wetu
wa nyumbani,” anasema Aurora.
0 maoni:
Chapisha Maoni