Jumanne, 15 Oktoba 2013









Yondani: Beki wa kati asiye na mpinzani Ligi Kuu Bara


NANI asiyefahamu makali ya Kelvin Patrick Yondani ‘Vidic’ wa Yanga anapokuwa kwenye himaya yake ya ulinzi ambapo  sasa anahesabika kuwa ndiye beki bora wa kati Tanzania.
Uimara wa Yondani ndiyo umemfanya apewe jina la Vidic wakimfananisha na beki wa Manchester United, Nemanja Vidic na yeye ndiye beki anayempenda.

Yondani ameufanya ukuta wa Yanga kusimama imara hadi sasa akishirikiana na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na msimu uliopita walitwaa taji la Ligi Kuu Bara na yeye akatangazwa mchezaji bora wa mwaka.

Ana umbo la kawaida, lakini sifa yake kubwa ni kucheza mipira ya juu kwa kichwa, anatumia akili kwenye kukaba, ni mwiba wa kuogopwa na mastraika wakorofi.
Yondani anasema siri ya yote hayo ni mazoezi, kufuata maelekezo ya kocha na ushirikiano wake na wachezaji wenzake kikosini.

“Kila kitu ni kujituma, nashukuru Mungu kwa yote, yeye ndiye kila kitu, ndiye aliyenijalia yote,”anasema.
Kikosi cha Yanga kwa sasa hasa safu ya beki wa kati ina ushindani ingawa Kocha Mkuu, Ernest
Brandts ameendelea kuwaamini, Yondani na Cannavaro. Wapo wengine, Rajab Zahir, Ibrahim Job, Issa Ngao na Mbuyu Twite anayetumika kama beki wa kulia.
Yondani anasema: “Mafanikio yoyote lazima ukutane na changamoto, ndipo utajua kipimo cha nguvu yako.”

“Kweli katika nafasi ya beki wa kati tupo wengi, lakini ukweli utabaki pale pale anayejua ndiye atakayepata nafasi ya kucheza,”anaeleza Yondani.

“Ushindani unakufanya mchezaji ujipange na kutobweteka, unapokosa mshindani unabweteka na kufikiri nitapangwa tu. Lakini ushindani unakufanya ujitambue na kujipanga uwe vizuri kila siku kwani ukilala kidogo tu, mwana si wako tena.”

Kuhusu uchezaji bora wa ligi msimu huu baada ya kupata msimu uliopita, Yondani anasema: “Ndiyo tuko kwenye ngoma tunacheza, ligi inaendelea lakini mawazo yangu ni kujituma kuipa mafanikio

Yanga.”
“Nitajitahidi kadri niwezavyo tufanikiwe na mambo mengine ya uchezaji bora, huwa yanafuata tu, ni mipango ya Mungu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

0 maoni:

Chapisha Maoni

Item Reviewed: Description: Rating: 5 Reviewed By: Unknown
Scroll to Top